Imarati yawalipa magaidi mamilioni ya dola kumuokoa mwanamfalme
-
Imarati yawalipa magaidi mamilioni ya dola kumuokoa mwanamfalme
Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) imewalipa magaidi wa al-Qaeda zaidi ya dola milioni 23 kama kikomboleo cha mwanamfalme aliyekuwa ametekwa nyara na magaidi hao huko Mali, magharibi mwa Afrika.
Shirika la Habari la Fars limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa watawala wa Muungano wa Falme za Kiarabu wamewalipa magaidi hao wenye mfungamano na al-Qaeda fedha taslimu, dola milioni 23 za Kimarekani ili wamwachilie huru Ahmed bin Maktoum bin Juma Al Maktoum, mmoja wa watu wa familia ya kifalme ya utawala wa Dubai, mwenye umri wa miaka 78.
Ahmed bin Maktoum alitekwa nyara mwezi Septemba mwaka huu wakati watu wenye silaha walipovamia shamba lake kusini mwa Bamako, mji mkuu wa Mali. Kwa mujibu wa maafisa kadhaa wa nchi za Magharibi, baada ya kutekwa nyara mwanamfalme huyo wa utawala wa Dubai alisafirishwa hadi Bamako na kulianza mfululizo wa mazungumzo ya siri baina ya maafisa wa Mali na wapatanishi kadhaa wa eneo hilo mpaka magaidi hao walipokubali kumwachia huru Ahmed bin Maktoum kwa kikomboleo cha dola milioni 23, fedha taslimu.
Duru za kuaminika zimesema kwamba makubaliano hayo yamejumuisha pia kuachiliwa huru wafungwa kadhaa wanaohusiana na magenge ya kigaidi yenye msimamo mkali nchini Mali.
Magaidi hao wameachiliwa huru kwa ombi la genge hilo la kigaidi lenye nguvu na ambalo lenyewe limetangaza kuwa licho chini ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika eneo la Sahel la Afrika. Hivi sasa genge hilo limedhibiti sehemu kubwa za kaskazini na katikati mwa Mali na linatuhumiwa kuwa linaungwa mkono na wakoloni wa Ufaransa ambao wametimuliwa nchini Mali.