Iran yatangaza kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita na Marekani
Sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) imethibitisha kuwa Iran na Marekani zimekamilisha maandishi ya hati ya makubaliano (MoU) yanayolenga kumaliza vita, kusimamisha mara moja na kwa kudumu operesheni zote za kijeshi katika nyanja zote, ikiwemo Lebanon, na pia kuondoa mzingiro wa baharini uliowekwa na Marekani dhidi ya Iran.
Katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo, sekretarieti ya SNSC ilisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, chini ya mwongozo wa Kiongozi wake shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kwa maelekezo ya Kiongozi wa sasa Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, kwa uungwaji mkono thabiti wa wananchi wa Iran, na kwa juhudi zisizokoma za vikosi vya ulinzi vya nchi hii, imefanikiwa kukamilisha kipindi kigumu cha mazungumzo ya kina na ya muda mrefu.
Taarifa hiyo imesema: “Kwa mujibu wa idhini ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, maandishi ya hati ya makubaliano kuhusu mazungumzo ya kumaliza vita, yajulikanayo kama mazungumzo ya Islamabad, kati ya Iran na Marekani yamekamilishwa jioni ya tarehe 14 Juni,”
“Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, vita na operesheni zote za kijeshi katika pande zote, ikiwemo Lebanon, zitasitishwa mara moja na kwa kudumu. Aidha, mzingiro wa baharini dhidi ya Iran utaondolewa mara moja na kikamilifu.”
Sekretarieti hiyo imeongeza kuwa hati hiyo ya makubaliano inatarajiwa kutiwa saini rasmi siku ya Ijumaa, tarehe 19 Juni.
Aidha imeelezwa kuwa mazungumzo kuelekea kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho yataahirishwa hadi pale upande wa pili utakapotekeleza kikamilifu ahadi zake zilizoainishwa katika hati hiyo.
Taarifa hiyo pia ilitoa shukrani kwa Pakistan na Qatar kwa juhudi zao za upatanishi zilizosaidia kufanikisha mazungumzo hayo.
Tangazo hilo linakuja kufuatia uthibitisho wa awali uliotolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharibabadi pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif.
Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump alikaribisha hatua hiyo kupitia jukwaa lake la Truth Social, akitoa idhini ya kuondolewa kwa mzingiro huo wa baharini.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kutiwa saini nchini Uswisi.
Wakati huo huo, makao makuu ya uongozi wa vikosi vya ulinzi vya Iran yamesema kuwa azma na msimamo wa taifa la Iran ni nukta ambazo zimewalazimisha maadui kukubali hali halisi ya uwanja wa mapambano.
Katika taarifa iliyotolewa mapema Jumatatu, Kamandi ya Khatam al‑Anbiya imewapongeza wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ushindi wenye fahari.
Taarifa hiyo pia imewapongeza wanajeshi wa vikosi vya ulinzi pamoja na wanachama wa mhimili wa muqawama kwa “uthabiti wao usiotikisika” katika kipindi cha zaidi ya siku 100 za vita.
Aidha taarifa hiyo imesema“Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu na chini ya uongozi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi wa Iran pamoja na wapiganaji wao wameonyesha wazi kuwa maadui yaani Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israeli hawana budi ila kukubali kushindwa na kusalimu amri."
Aidha taarifa hiyo imesema “mapenzi ya Mwenyezi Mungu na azma ya chuma” ya taifa la Iran sasa ni “ngome isiyovunjika” dhidi ya aina zote za uchokozi, na njia ya muqawama inaendelea kuwa ndiyo njia pekee ya kufikia ushindi.
Ikumbukwe kuwa tawala za Marekani na Israel zilianzisha vita dhidi ya Iran 10 Ramadhani sawa na Februari 28 mwaka huu kwa kumuua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, makamanda wa ngazi za juu wa kijeshi, watoto wa sule na raia wa kawaida. Vita hivyo viliendelea kwa muda wa siku 40 ambapo Iran ilitekeleza mawimbi 100 ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa kulenga ngome za kijeshi na kiuchumi za Marekani na Israel kote katika eneo la Asia Magharibi. Maadui hao wawili walilazimika kuomba usitishaji vita kutokana na vipigo walivyopokea kutoka vikosi vya Iran.