Jenerali mstaafu Nigeria afariki akiwa ametekwa, rais aapa kuchukua hatua kali
-
Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu
Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ameapa kuangamiza wale aliowataja kuwa ni “maadui wakubwa” wa nchi hiyo baada ya jenerali mstaafu wa jeshi kufariki dunia akiwa mikononi mwa watekaji nyara.
Rais Tinubu amebainisha kushtushwa na kifo cha Meja Jenerali mstaafu Rabe Abubakar, ambaye alitekwa nyara pamoja na mkewe katika jimbo la Katsina walipokuwa wakielekea katika mji wao wa asili. Rais Tinubu ametoa pole kwa familia ya marehemu huku akiahidi kuwa atachukua hatua kali kukabiliana na watekaji nyara hao.
Jenerali huyo mstaafu alitekwa nyara pamoja na mkewe, Hajiya Amina Abubakar, walipokuwa wakisafiri kupitia jimbo la Katsina mwishoni mwa mwezi uliopita.
Mke wa marehemu jenerali bado anashikiliwa na hali yake haijafahamika.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi kuthibitisha kifo cha Abubakar, serikali ya jimbo la Katsina ilisema kuwa afisa huyo wa zamani wa ngazi ya juu jeshini alifariki kutokana na sababu zinazohusiana na “madhara ya kiafya” yaliyotokana na ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu alipokuwa matekani.
Siku chache baada ya utekaji huo, watekaji walitoa video ikionyesha wanandoa hao wakiwa mikononi mwao.
Katika video hiyo, mke wa jenerali mstaafu aliomba serikali iingilie kati, huku akieleza baadhi ya madai ya watekaji nyara, yakiwemo kuachiliwa kwa wanachama watatu wa kundi lao wanaoshikiliwa na mamlaka za usalama.
Pia walidai kurejeshewa mifugo wanayodai ilitaifishwa kutoka kwao. Hakukuwa na malipo ya fedha kama kikomboleo katika video hiyo.
Rais Tinubu alisema kuwa ingawa “magaidi wamefanya mabaya yao makubwa,” serikali yake “haitawahi kukubali shinikizo lao la kutaka wanachama wao wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama waachiliwe.”
Marehemu Jenerali Abubakar alihudumu katika jeshi la Nigeria tangu mwaka 1989, akishika nyadhifa kadhaa za juu, zikiwemo kuwa msemaji wa jeshi kati ya mwaka 2015 na 2017 alipostaafu.
Jimbo la Katsina ni miongoni mwa maeneo kadhaa nchini Nigeria yaliyoathiriwa vibaya na matukio ya utekaji nyara yanayofanywa na makundi yenye silaha. Watekaji hao mara nyingi hulenga jamii za vijijini, wasafiri, na taasisi za elimu, wakiteka watu ili kudai kikomboleo.
Katika baadhi ya matukio yaliyopita, watekaji waliwaua mateka wao pale ambapo madai yao ya vikomboleo hayakutimizwa. Nigeria pia imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya makundi ya kigaidi, yakiwemo Boko Haram na Daesh.