Oct 06, 2024 07:27 UTC
  • ICC yatoa hati ya kuwakamata washukiwa 6 nchini Libya

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetoa hati ya kukamatwa wanaume sita wanaodaiwa kuhusishwa na wanamgambo katili wa Libya wanaotuhumiwa kwa mauaji mengi na uhalifu mwingine katika mji muhimu wa magharibi mwa Libya ambapo makaburi ya halaiki yaligunduliwa mnamo 2020.

Mwendesha Mashtaka wa ICC, Karim Khan amesema uchunguzi wake umekusanya ushahidi "unaoonyesha kwamba wakazi wa Tarhunah wamekabiliwa na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji, uvunjaji wa utu wa mtu, ukatili, mateso, unyanyasaji wa kingono na ubakaji."

Kibali cha Mahakama kinataka kukamatwa watu sita ambao ni: Abdelrahim al-Kani, Makhlouf Douma, Nasser al-Lahsa, Mohammed Salheen, Abdelbari al-Shaqaqi na Fathi al-Zinkal.

Mwendesha mashtaka wa ICC, Karim Khan amesema kuwa watatu kati ya washukiwa hao walikuwa viongozi au wanachama wakuu wa wanamgambo wa Al Kaniyat ambao walidhibiti Tarhunah tangu 2015 hadi Juni 2020, na wengine watatu walikuwa maafisa wa usalama wa Libya waliohusishwa na makundi ya wanamgambo wakati wa uhalifu huo.

Karim Khan

Makaburi ya halaiki yaligunduliwa huko Tarhunah baada ya wanamgambo hao kuondokka eneo hilo kufuatia kusambaratika kwa kampeni ya miezi 14 ya kamanda wa kijeshi, Khalifa Hifter, ya kutaka kudhibiti mji wa Tripoli kutoka kwa kundi la wanamgambo waliokuwa wakishirikiana na serikali ya zamani inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Mahakama ya ICC haina jeshi la polisi na inategemea ushirikiano kutoka kwa nchi 124 wanachama kutekeleza hati za kukamatwa kwa washukiwa hao.