Oman: Badala ya kulaani hatua ya Iran, komesheni Israel kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina
(last modified 2024-10-05T03:44:17+00:00 )
Oct 05, 2024 03:44 UTC
  • Oman: Badala ya kulaani hatua ya Iran, komesheni Israel kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman amesema, badala ya kulaani hatua ya Iran, ukomeshwe ukaliaji ardhi ya Palestiina kwa mabavu unaofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Seyyed Badr Albusaidi, ameyasema hayo katika ujumbe alioweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, alipojibu shutuma zinazotolewa dhidi ya jibu halali la kijeshi la Iran kwa hatua za kichokozi na za kigaidi za utawala wa Kizayuni kupitia operesheni ya Ahadi ya Kweli 2 .
 
Amefafanua kwa kusema: "ni rahisi kwa serikali fulani kusimama na kulaani vitendo vya Iran. Lakini hiyo haitatui chochote, wala vyovyote itakavyokuwa, sera iliyozoeleka ya kuitetea Israel . Badala yake tunapaswa kushughulikia sababu halisi ya mgogoro uliopo. Hiyo ina maana ya kuukabili ukweli usiokanushika kwamba ni kwa kukomesha ukaliaji haramu wa ardhi unaofanywa na Israel dhidi ya Palestina ndipo tutaweza kuwa na matumaini ya kurejesha amani katika eneo. Yeyote anayeamini kwamba tunaweza kupata amani kwa njia nyinginezo - kwa kuidhibiti Iran, kwa kuifuta Hamas, kwa kuishinda Hizbullah, au kwa kutoa usaidizi na uungaji mkono thabiti wa kisiasa, kijeshi na kifedha kwa Israel - ama atakuwa amehadaika, ni mjinga au anajaribu kwa makusudi kukwepa ukweli".
Seyyed Badr Albusaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ameendelea kusema: "ni vigumu kuukubali ukweli katika hali hii. Kwa muda mrefu sana serikali nyingi za Magharibi zimeakhirisha kuuzingatia ukweli huu na kushindwa kuwahakikishia watu wa Palestina usalama na utulivu unaoweza kudhaminiwa na kuwa na dola kamili tu. Haki na maisha ya watu wa Palestina wanaokaliwa ardhi yao yamekuwa yakimomonyoka hatua kwa hatua kutokana na upanuzi wa vitongoji haramu na kutwisha utawala wa kibaguzi wa Apathaidi. Waungaji mkono wa Israel wanazungumza kwa kutumia jina la sheria za kimataifa huku wakizuia mara kwa mara utekelezaji wake katika kadhia ya Palestina. Hii ni lazima ibadilike hivi sasa hivi. Kuheshimu sheria ya kimataifa lazima kuwe kwa dhati si kwa maneno bali kwa vitendo. Israel lazima itakiwe kusimamisha operesheni zake za kijeshi huko Ghaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Lebanon. Hili linapaswa kufuatwa na hatua za pamoja za kimataifa za kukomesha Israel kuikalia kwa mabavuu ardhi ya Palestina. Taifa lenye mamlaka kamili la Palestina lazima lianzishwe, likiungwa mkono sio tu na maandishi ya sheria bali na nyenzo zote za kitaasisi na kijumuiya za Jamii ya Kimataifa.

 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ametangaza msimamo huo wakati hali ya wasiwasi imezidi kutanda katika eneo la Asia Magharibi sambamba na kukaribia kumbukumbu ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa tarehe 7 Oktoba 2023 na harakati ya Hamas katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na ambayo imetumiwa na utawala wa Kizayuni kama kisingizio cha kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza kwa lengo lililotangazwa kuwa eti ni "kuiangamiza Hamas".
 
Siku ya Jumanne jioni (tarehe 1 Oktoba 2024), makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC yalitwanga shabaha kwenye vituo vya usalama na kijasusi vya utawala wa Kizayuni kupitia operesheni ya Ahadi ya Kweli 2 iliyotekelezwa kwa kaulimbi ya "Yaa RasulaLlah".

Kufanikiwa kwa asilimia 90 shambulio hilo kupiga maeneo yaliyokusudiwa kumethibitisha uwezo kamili wa kunasa taarifa na wa utekelezaji wa operesheni ya kijeshi ilionao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kuutiwa kiwewe utawala wa Kizayuni.../

Tags