IRGC: Vikosi vya Ulinzi vya Iran viko tayari kujibu tishio lolote dhidi ya Iran
(last modified 2024-10-21T11:39:32+00:00 )
Oct 21, 2024 11:39 UTC
  • IRGC: Vikosi vya Ulinzi vya Iran viko tayari kujibu tishio lolote dhidi ya Iran

Naibu Kamanda wa Uratibu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesisitiza kuwa vikosi vya ulinzi vya nchi hii vimejiandaa kikamilifu kujibu tishio lolote dhidi ya nchi hii kufuatia kupamba moto mivutano katika eneo.

Brigedia Jenerali Iraj Masjedi amesema kuwa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimejiandaa kikamilifu kila siku kukabiliana na tishio dhidi ya ardhi ya Iran. 

Akizungumzia ushiriki mkubwa wa Wairani katika hafla ya mazishi ya Meja Jenerali Abbas Nilfuroushan, kamanda mwandamizi wa IRGC ambaye aliuawa shahidi mwezi uliopita akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika shambulio la anga la Israel dhidi ya nchi hiyo, Brigedia Jenerali Masjedi amesema hamasa hiyo imethibitisha azma na kuwa tayari wananchi kuendeleza njia ya mashahidi.

"Hatutarudi nyuma mkabala wa kuuliwa shahidi makamanda wetu; na tutalipiza kisasi kwa Wazayuni kwa kumwaga damu ya mashahidi wetu wapendwa na wananchi madhulumu wa Palestina," amesema Kamanda Iraj Masjedi.

Tel Aviv imetishia kuishambulia Iran, na Tehran imeapa kutoa jibu la "kuangamiza" mkabala wa chokochoko zozote dhidi yake. 

Jana Jumapili Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, shambulio lolote litakalofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu litajibiwa vikali na kwamba, maeneo yote ya Israel yanayopaswa kupigwa kwa silaha za Iran, yameshaainishwa.

 

Tags