Mkuu wa Umoja wa Afrika alaani ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji
(last modified 2024-10-21T11:47:15+00:00 )
Oct 21, 2024 11:47 UTC
  • Mkuu wa Umoja wa Afrika alaani ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat leo Jumatatu amelaani mauaji ya viongozi wawili wa upinzani nchini Msumbiji na kutaka uchunguzi ufanyike ili wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Watu wenye silaha juzi Jumamosi walimuua kwa risasi Elvino Dias Wakili wa Venancio Mondlane mgombea urais wa chama cha upinzani cha Podemos.

Venancio Mondlane, mgombea wa kiti cha urais wa upinzani

Paulo Guambe afisa wa chama cha Podemos pia aliuawa pamoja na Dias wakati watu waliokuwa na silaha walipoifyatulia risasi gari yao katika mji mkuu Maputo. 

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) amewataka maafisa usalama wa Msumbiji kufanya uchunguzi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa mauaji hayo. 

Chama cha Podemos kimepinga matokeo ya uchaguzi ambayo yameonyesha kuwa chama tawala cha Msumbiji, Frelimo ambacho kimekuwa madarakani kwa nusu karne tangu uhuru,  kinaongoza.

Ingawa kura bado zinahesabiwa katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika, Mondlane amedai kuwa ameshinda uchaguzi huo.

Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu wa Msumbiji yanatazamiwa kutangazwa wiki hii. 

Akitoa wito wa utulivu, mkuu huyo wa Umoja wa Afrika amesema anaendelea kufuatilia kwa karibu matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Msumbiji na kueleza wasiwasi wake kuhusu visa vilivyoripotiwa vya ghasia za baada ya uchaguzi na hasa mauaji ya hivi karibuni.

Raia wa Msumbiji wasiopungua milioni 17 waliojiandikisha kupiga kura tarehe 9 mwezi huu walielekea katika vituo vya kura kwa lengo la kumchagua rais mpya, wawakilishi wa bunge na magavana wa majimbo ya nchi hiyo katika uchaguzi unaotazamiwa kwa kiasi kikubwa kukibakisha madarakani chama tawala cha FRELIMO ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 49 sasa.

Tags