Kuendelea maandamano dhidi ya Netanyahu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel)
(last modified 2024-10-20T13:26:10+00:00 )
Oct 20, 2024 13:26 UTC
  • Kuendelea maandamano dhidi ya Netanyahu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel)

Maandamano dhidi ya Benjamin Netanyahu ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yamepelekea kuibuka vuta nikuvute na makabiliano kati ya waandamanaji na polisi.

Maelfu ya watu walifanya maandamano tena Jumamosi ya jana mbele ya Wizara ya Vita ya utawala wa Kizayuni kwa minajili ya kuunga mkono mpango wa kubadilishana wafungwa na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina "HAMAS" na kutoa nara dhidi ya Netanyahu. Vikosi vya polisi vya utawala wa Kizayuni vilipambana na waandamanaji hao waliokuwa na hasira na idadi kubwa ya waandamanaji pia walitiwa mbaroni.

Licha ya uingiliaji kati wa polisi, waandamanaji wenye hasira walielekea Caesarea yalipo makazi ya Netanyahu huko Tel Aviv. Wakiwa wamebeba mabango na maberamu, waandamanaji hao walimshutumu Benjamin Netanyahu kwa kufanya mauaji dhidi ya  watoto wao.

Anga na mazingira yanayotawala hivi sasa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu imekuwa mbaya sana katika wiki za hivi karibuni na maandamano ya mitaani dhidi ya Netanyahu na baraza lake la mawaziri yameshika kasi na kuchukua wigo mpana zaidi. Waandamanaji hukusanyika kila siku dhidi ya Netanyahu, na matakwa yao makubwa kwa utawala wa Kizayuni ni kukubali kusimamisha mapigano na kubadilishana mateka wa Kizayuni na Hamas.

 

Maandamano makubwa  dhidi ya Benjamin Netanyahu  huko Tel Aviv

Katika miezi ya hivi karibuni, Netanyahu ameendelea na hatua zake za kivita kwa kuahidi kuitimua Hamas kutoka Ukanda wa Gaza na kuangamiza kabisa makundi ya muqawama wa Palestina. Sambamba na hayo, hali ya mvutano kati ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na wajumbe wengine wa baraza la mawaziri imeendelea na kusababisha kuongezeka mashambulizi ya kinyama dhidi watu wa Ukanda wa Gaza na kupelekea kushadidi kwa ukosefu wa utulivu katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.

Baraza la mawaziri la muungano la utawala wa Kizayuni linaundwa na makundi mawili ya wapenda vita na Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada, na hitilafu baina ya makundi hayo mawili kuhusiana na kuendelea vita huko Ukanda wa Gaza zimeongezeka kutokana na kushindwa mtawalia jeshi la utawala huo katili huko Gaza dhidi ya makundi ya Muqawama wa Palestina.

Licha ya indhari na maonyo ya baadhi ya viongozi wa Kizayuni, lakini Wazayuni wenye kufurutu ada wanaunga mkono kuendelea vita huko Gaza katika hali ambayo mamlaka za kiusalama na kijeshi za utawala wa Kizayuni zinatahadharisha vikali kuhusu madhara makubwa ya vita hivyo na ongezeko la mgogoro huko Tel Aviv.

 

Kuendelea kwa maandamano makubwa  katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu dhidi ya Netanyahu

Matokeo ya uchochezi wa vita wa mamlaka ya Kizayuni yamekuwa na madhara makubwa katika uchumi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kivitendo, kuendelea kukosekana utulivu kumeyafanya makampuni ya Magharibi kutokuwa tayari tena kuendelea na shughuli zao huko Tel Aviv.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kuendelea vita vya Ukanda wa Gaza katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kumesababisha kushadidi mgogoro wa kiuchumi, kiusalama na kisiasa, na hitilafu za ndani kati ya Wazayuni pia zimeongezeka sana.

Hatua ya Netanyahu ya kuwa pamoja na Wazayuni wenye misimamo ya kuchupa mipaka na kuvurugwa mchakato wa mazungumzo ya usitishaji vita kumepelekea kushadidi maandamano ya familia za mateka wa Kizayuni wanaomshutumu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ndiye mhusika mkuu wa hali mbaya inayoshuhudiwa hivi sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Mgogoro wa kiuchumi pia ndio sababu kuu ya malalamiko zaidi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na ukosefu wa uthabiti wa ndani wa utawala wa Kizayuni utaongezeka kwa kuendelea vita vya Ukanda wa Gaza.

Matarajio ya matukio ya siku za usoni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, pamoja na kuendelea kwa hali ya sasa yatasababisha migogoro ya ndani ya Tel Aviv na hatimaye kuporomoka vibaya kwa utawala huo katili wa Israel.

Kuendelea siasa za kupenda vita huko Ukanda wa Gaza kunakwenda sambamba na matakwa ya Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada ambao hawakubali mazungumzo ya usitishaji vita kwa hali yoyote ile. Katika hali na mazingira kama haya, Baraza la Mawaziri la Netanyahu ambalo kimsingi limekalia kuti kavu litakabiliwa na msambaratiko na hata kufanyika uchaguzi wa mapema hatakuwa mwarobaini na tiba mujarabu ya kuhitimisha mgogoro wa ndani katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Tags