Hizbullah yafanya mashambulio makubwa dhidi ya vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni
(last modified 2024-10-20T06:47:03+00:00 )
Oct 20, 2024 06:47 UTC
  • Hizbullah yafanya mashambulio makubwa dhidi ya vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni

Katika kuendeleza operesheni zake za kuzuia hujuma, Hizbullah ya Lebanon imefanya mashambulio makali ya makombora na mizingia yaliyolenga ngome za Wazayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).

Kulingana na shirika la habari la  IRNA, harakati ya Muqawama wa  Kiislamu ya Lebanon imetangaza katika taarifa kuwa, vikosi vya Hizbullah vimekilenga kitongoji cha Rosh Bina kilichoko kusini mashariki mwa mji wa Safad kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa mashambulizi makali ya makombora na mizinga.

Hizbullah imeendelea kueleza katika taarifa hiyo kwamba imewalenga pia wanajeshi wa Kizayuni karibu na lilipo ingilio la Shabaa katika kitongoji cha al-Manarah.

Kiryat Ata, iliyoko mashariki mwa Haifa pia ni miongoni mwa maeneo ambayo yamelengwa na mashambulizi ya makombora  ya Hizbullah ya Lebanon.

Wimbi hili la mashambulizi ya makombora  ya Hizbullah linatokea baada ya kufanikiwa shambulio la ndege zisizo na rubani za harakati hiyo lililolenga makazi ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu.

Mashambulio ya Hizbullah ya Lebanon yanayofanywa kwa ajili ya kuunga mkono Muqawama wa Ukanda wa  Gaza na kujibu mashambulio  ya utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya raia wa kusini mwa Lebanon yamekuwa jinamizi kwa walowezi wa Kizayuni, ambao kwa miezi kadhaa sasa wamekuwa wakikimbilia mafichoni kutoka maeneo ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Tags