Kamati ya Bunge la Iran: Kuuawa shahidi Sinwar kutaharakisha maangamizi ya Israel
(last modified 2024-10-20T02:47:39+00:00 )
Oct 20, 2024 02:47 UTC
  • Kamati ya Bunge la Iran: Kuuawa shahidi Sinwar kutaharakisha maangamizi ya Israel

Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa, damu takasifu ya Shahidi Yahya Sinwar itasafisha zaidi njia ya kuikomboa Quds na kuharakisha maangamizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Yahya Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS aliuawa shahidi siku ya Jumatano ya tarehe 16 Oktoba wakati akipambana na adui ghasibu wa Kizayuni katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Wanachuo wa Iran (ISNA), Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje ya Bunge la Iran imetoa taarifa kufuatia kuuawa shahidi Sinwar na kueleza kwamba kiongozi huyo wa Hamad alikuwa shakhsia jasiri, shujaa na asiyechoka wa Hamas na Kambi ya Muqawama na ruwaza na kigezo kamili cha subira, Muqawama na usimamaji imara katika ulimwengu wa zama hizi.
Bunge la Iran

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, miaka zaidi ya 20 ya kusota jela na kushikiliwa mateka katika gereza la utawala dhalimu na katili wa Kizayuni na genge la wahalifu na watenda jinai waliokubuhu kwa unyama kuwapita madikteta na wanyonya damu wote duniani, ni sehemu tu ya jihadi kubwa ya shahidi huyo aliyetukuka, ambaye hata katika pumzi za mwisho za uhai wake alisimama kiume pia katikati ya medani ya mapigano pasi na kuiacha bendera ya mapambano idondoke chini.

Mbali na kulaani mauaji ya Yahya Sinwar, ambayo ni sehemu ya jinai zisizo na mfano kuwahi kufanywa na utawala wa Israel katika miezi ya hivi karibuni na mauaji ya kimbari yaliyopangwa na kuratibiwa na genge hilo la uhalifu, Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje ya Bunge la Iran imewaonya waungaji mkono wa utawala huo ghasibu na muuaji wa watoto wadogo kwamba waache kuiunga mkono Israel haraka iwezekanavyo na kutozidi kuwa washirika wa uhalifu wa kutisha unaofanywa na utawala huo bandia.../