Juhudi za Wazayuni za kuzuia jinai zao huko Gaza zisisajiliwe, waandishi habari wanashambuliwa
(last modified 2024-10-21T07:17:42+00:00 )
Oct 21, 2024 07:17 UTC
  • Juhudi za Wazayuni za kuzuia jinai zao huko Gaza zisisajiliwe, waandishi habari wanashambuliwa

Miongoni mwa mistari myekundu ambayo Wazayuni wamepuuza na kuvuka katika mashambulizi ya kikatili na ya kinyama huko Gaza na Lebanon ni kulenga waandishi wa habari.

Tangu mwanzoni mwa uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza, maafisa wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakieleza kwamba, Israel inafanya jinai za kivita na dhidi ya binadamu katika eneo hilo la Palestina. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanakiri kwamba, hakuna jinai yoyote dhidi ya binadamu ambayo haijafanywa na Wazayuni katika Ukanda wa Gaza.

Mfano wa karibuni zaidi ni mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya waandishi wa habari. Akizungumzia mashambulizi dhidi ya vyombo vya habari na mauaji ya kupanga dhidi ya makumi waandishi wa habari katika Ukanda wa Gaza katika mwaka uliopita, Irene Khan, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, amesisitiza kuwa uhuru wa kujieleza umekuwa hatarini zaidi katika vita vya Gaza kuliko vita vingine vya hivi karibuni.

Ripota Maalumu wa UN amesema: Inaonekana kwamba kupigwa marufuku shughuli za televisheni ya Al-Jazeera, na kuzidishwa udhibiti na uchujaji wa habari katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel) vinaakisi mkakati wa maafisa wa Israel wa kunyamazisha waandishi habari wakosoaji na kuzuia utunzaji wa kumbukumbu za uhalifu wa kimataifa.

Israel imeua makumi ya waandishi habari katika Ukanda wa Gaza

Irene Khan pia amekosoa vikali 'ubaguzi na sera za undumakuwili' ambavyo vimesababisha vikwazo na kukandamizwa maandamano na hotuba za Wapalestina katika sehemu tofauti za dunia. Katika matamshi yake, Khan ameashiria marufuku kama hizi nchini Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya, ukandamizaji mkali wa maandamano katika maeneo ya vyuo vikuu vya Marekani, na marufuku ya alama na kauli mbiu za kitaifa za Palestina ambazo zimetambuliwa kuwa ni kosa na uhalifu katika baadhi ya nchi. Ripota huyo Maalumu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa: "Wakati majukwaa ya mitandao ya kijamii yamekuwa njia ya mawasiliano kutoka na kuelekea Gaza, tumeshuhudia ongezeko la taarifa zisizo za kweli, uenezaji wa uongo na maneno ya chuki katika vyombo vya habari. Watu wa Gaza hawakukabiliwa tu na uvunjaji wa haki na uhalifu mkubwa wa Wazayuni, bali pia wamekuwa shabaha ya vita vya kisaikolojia vya washirika wa utawala wa Kizayuni wa Kimagharibi."

Katika vita hivi vya kisaikolojia, Marekani na serikali za nchi za Ulaya zinazodai kutetea haki za binadamu zimemuweka katili muuaji sehemu ya mhanga na mdhulumiwa. Wanasimulia uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Gaza isivyo na kwa kupindua ukweli wa mambo, kana kwamba Wazayuni watenda jinai ndio wahanga, na wanawake na watoto wa Kipalestina ni magaidi wauaji!

Hatua ya kwanza ya Wazayuni katika vita hivyo vya kisaikolojia dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina ni kuwalenga waandishi wa habari na kuzuia utayarishaji na utunzaji wa nyaraka na ushahhidi wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Palestina. Katika mwaka uliopita, makumi ya waandishi wa habari wa Kipalestina na wasio Wapalestina walilengwa kwa risasi za moja kwa moja za wanajeshi wa Israel. 

Irene Khan, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, amesisitiza kwamba "katika zama za hivi karibuni hakuna mzozo ambao umetishia sana uhuru wa kujieleza kama wa Gaza" na kufafanua kuwa, kushambua vyombo vya habari ni shambulio dhidi ya haki ya kila mtu duniani ambaye anataka kujua kinachojiri.

Katibu Mkuu wa zamani wa Amnesty International amesema kuhusu unafiki na undumakuwili wa nchi za Magharibi katika kukabiliana na jinai za Wazayuni huko Gaza kwamba: "Ujumbe wangu mkuu ni kwamba, yanayotokea Gaza yanatoa ishara kwa dunia nzima kwamba ni sawa kufanya mambo kama haya, kwa sababu yanafanyika huko Gaza, na Israel inapewa kinga na kukingiwa kifua kinga kikamilifu; hivyo pande nyingine kote duniani zitaamini kuwa zitapewa kinga kamili."

Viongozi wa mataifa ya Magharibi wanakanusha kutokea jinai yoyote huko Gaza licha ya maafisa wa Umoja wa Mataifa, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kukiri kwamba, kunafanyika mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Katika mwaka uliopita, zaidi ya watu 42,000 wa Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi. Karibu watu laki moja wamejeruhiwa, milioni mbili wamelazimika kuhama makazi yao na wanazingirwa kikamilifu na jeshi la Israel wakisumbuliwa na njaa na kiu. Je, vitendo hivi si mauaji ya kimbari?