Watumiaji wa mitandao nchini Misri wafurahishwa na Araqchi kuagiza chakula mkahawani huko Cairo
(last modified 2024-10-21T11:30:25+00:00 )
Oct 21, 2024 11:30 UTC
  • Watumiaji wa mitandao nchini Misri wafurahishwa na Araqchi kuagiza chakula mkahawani huko Cairo

Wananchi wa Misri mitandaoni wamefurahishwa na kitendo cha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran cha kuagiza chakula katika mkahawa mmoja katika mji mkuu wa nchi hiyo Cairo pambizoni mwa ziara yake ya karibuni nchini humo.

Sayyid Abbas Araqchi alikwenda katika mkahawa mmoja katika eneo la al Balad katika mji mkuu wa Misri, Cairo na kuagiza chakula cha asili cha watu wa Misri kwa jina la al Koshari; kitendo ambacho kimefurahiwa na kupokelewa vyema na watumiaji wa mitandao ya kijamii wa Misri.

Chakula cha asili cha watu wa Misri cha al "Koshari"

Shirika la habari la ISNA limeripoti kuwa, hatua ya Araqchi ya kuagiza chakula katika mkahawa huo ambayo imefafanuliwa katika mfumo wa "diplomasia ya watu", imeakisiwa na kuzingatiwa pakubwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii huko Misri.  

Idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Misri walimwomba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ajaribu kula pia chakula cha nchi hiyo kwa jina la "Felafel" na kile kinachojulikana kama "Ful." 

Ni vyema kueleza hapa kuwa "Al-Koshari", ni sahani maarufu ya chakula cha Wamisri ambacho huandaliwa kuchanganya mchele, adasi, dengu, njegere, pasta na viungo mbalimbali. 

Akiendelea na ziara yake ya kikanda mwishoni mwa wiki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwasili Amman mji mkuu wa Jordan na kisha akaelekea Cairo Misri kwa lengo la kushauriana na viongozi wa nchi mbalimbali za kanda hii kuhusu ulazima wa kusitishwa mauaji ya kimbari na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon. Sayyid Abbas Araqchi alikuwa na mazungumzo na mashauriano chanya na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi mbili hizo. 

Kama alivyoeleza mwenyewe mkuu wa chombo cha diplomasia wa Iran; moja ya mafanikio muhimu yaliyopatikana kufuatia mashauriano mtawalia yaliyofanywa katika kipindi hiki ni kufikiwa misimamo na kubainishwa wasiwasi wa pamoja mkabala wa mashambulizi na jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon.