Muqawama wa Iraq wafanya mashambulio ya ndege zisizo na rubani katika vituo vya Kijeshi vya utawala wa Kizayuni
(last modified 2024-10-21T07:45:26+00:00 )
Oct 21, 2024 07:45 UTC
  • Muqawama wa Iraq wafanya mashambulio ya ndege zisizo na rubani katika vituo vya Kijeshi vya  utawala wa Kizayuni

Katika taarifa, Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umetangaza kufanya mashambulio ya ndege zisizo na rubani katika maeneo ya utawala wa Kizayuni katika milima ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Israel.

Kundi la Muqawama wa Kiislamu la Iraq limetangaza kwamba, limeshambulia shabaha nyeti na muhimu ya utawala wa Kizayuni katika milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel kwa kutumia ndege isiyo na rubani.

Kundi hilo limesema kuwa, limefanya shambulio hilo kwa ajili ya kujibu mauaji na jinai za  kinyama  zinazofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya raia wakiwemo watoto, wanawake na wazee huko Gaza na Lebanon.

Taarifa hiyo inasisitizwa kuwa muqawama wa Kiislamu wa Iraq utaendeleza mashambulio yake dhidi ya ngome za adui Mzayuni hadi pale utakaposimamisha jinai zake dhidi ya raia wasio na hatia.

Hili ni shambulio la pili kufanywa na ndege zisizo na rubani za Muqawama wa Kiislamu wa Iraq dhidi ya vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel,  jana  Jumapili.

Muqawama wa Kiislamu wa Iraq, jana asubuhi pia, ulitangaza kushambulia kituo kingine muhimu cha utawala wa Kizayuni huko huko katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.  

Tags