Vijana wa Iraq wachoma moto ofisi ya kituo cha MBC cha Saudi Arabia
(last modified 2024-10-19T07:47:34+00:00 )
Oct 19, 2024 07:47 UTC
  • Vijana wa Iraq wachoma moto ofisi ya kituo cha MBC cha Saudi Arabia

Vijana wa Iraq waliokuwa na hasira wamechoma moto ofisi ya MBC ya Saudi Arabia mjini Baghdad baada ya kituo hicho cha televisheni kuwatusi makamanda wa muqawama waliouawa shahidi kuwa ni magaidi.

Katika kipindi chake cha wikendi, kanali ya MBC ya Saudia Arabia imewatuhumu viongozi wa Muqawama waliouawa shahidi kuwa ni magaidi kwa kutangaza ripoti iliyojaa matusi na uzushi.

Vijana wa Iraq wenye hasira kali wamechoma moto jengo hilo leo alfajiri (Jumamosi) katika kujibu matusi ya kanali hiyo ya MBC ya Saudia baada ya kuingia katika ofisi ya mtandao huo katika  eneo la Chuo Kikuu cha Baghdad na kuharibu vifaa vyake.

Kanali hiyo katika ripoti iliyorushwa hewani chini ya anwani ya "Milenia ya Kuondokana na Magaidi" imetukana na kuwavunjia heshima makamanda na viongozi mashahidi wa muqawama.

Katika taarifa yake, harakati ya Hamas imeeleza kuchukizwa kwake na hatua hiyo ya kanali ya Saudi Arabia na kuitaja kuwa ni kuanguka kimaadili na kuitaka iombe radhi.

Makundi ya Muqawama ya Iraq pia yametishia kushambulia ofisi ya kanali hiyo nchini Iraq ikiwa haitafungwa.
Yahya Sinwar, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) aliuawa shahidi siku ya  Jumatano,  tarehe 16, wakati akipigana na adui ghasibu wa Kizayuni katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Tags