Onyo la Iran kwa Marekani kuhusu chokochoko tarajiwa ya Israel
(last modified 2024-10-21T02:22:53+00:00 )
Oct 21, 2024 02:22 UTC
  • Onyo la Iran kwa Marekani kuhusu chokochoko tarajiwa ya Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Marekani inapasa kubebeshwa dhima ya shambulio lolote tarajiwa la Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii, Sayyid Abbas Araghchi ameeleza bayana kwamba, upande au mtu yeyote mwenye ufahamu wa jinsi na lini Israel itaishambulia Iran, anapaswa kuwajibishwa na kubeba dhima ya taathira hasi za shambulio hilo.

Akiashiria matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani, Joe Biden aliyesema kwamba alikuwa na wazo bora la jinsi na lini Israel itaishambulia Iran, Araghchi amesisitiza kuwa, yeyote atakayeunga mkono shambulio la Israel dhidi ya Iran awe tayari kuwajibikia jinai hiyo.

Oktoba Mosi, Iran ilivurumisha mamia ya makombora ya balestiki na kupiga kambi za kijasusi na kijeshi za utawala katili wa Israel, kama sehemu ya Operesheni ya Kweli ya Ahadi-2.

Baada ya shambulio la makombora la Operesheni ya Ahadi ya Kweli-2 lililofanywa na Iran kujibu jinai kubwa kama vile mauaji ya Ismail Haniyeh mjini Tehran, viongozi wapenda shari wa utawala haramu wa Israel wameahidi kuishambulia Iran eti kujibu Operesheni ya Kweli ya Ahadi 2 ya Jamhuri ya Kiislamu.

Utendaji huu kichokochoko na wa kivita wa Israel unafanyika kwa himaya na uungaji mkono wa wazi wa Marekani huku maafisa wa utawala wa Biden na yeye mwenyewe wakidai mara kwa mara haja ya kusimamishwa vita vya Gaza na kuhitimishwa mashambulizi dhidi ya Lebanon.

Joe Biden Rais wa Marekani

 

Hata hivyo matamshi ya hivi karibuni ya Rais Joe Biden kwamba, Marekani inafahamu ni lini na vipi uwezekano wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran yanaonyesha kwamba shambulio hili sio tu lina baraka zote za Washington bali lina himaya na na uungaji mkono kamili wa kisiasa na kijeshi wa dola hilo la kibeberu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kwa msaada wake kwa Israel kwa operesheni za kijeshi dhidi ya Gaza, Lebanon, na pengine Iran, Marekani ndio sababu kuu ya kuongezeka kwa mivutano na migogoro katika eneo la Asia Magharibi.

Katika hali ambayo, Marekani inadai kuwa inajaribu kuepusha vita katika eneo hili, lakini ni muungaji mkono mkuu wa kijeshi na silaha wa utawala wa Kizayuni, ambao unachukua hatua za makusudi katika mwelekeo wa kuchochea moto wa vita Asia Magharibi. Maafisa wa Marekani wanaunga mkono waziwazi vitendo vya kigaidi vya Israel na hii ina maana ya kumtia moyo mhalifu huyo kuendelea na jinai zake.

Kwa hakika, Israel itatumia zana na silaha za Marekani katika shambulio lolote tarajiwa dhidi ya Iran. Aidha, Tel Aviv ambayo hivi sasa iko katika hofu kubwa ya jibu la Iran, imeomba kutumwa mfumo wa Thaad dhidi ya makombora kutoka Marekani ili kama unavyodai uweze kukabiliana na mashambulio ya makombora ya Iran.

 

Katika hali ambayo Marekani ni mdhamini wa silaha zinazohitajika kwa utawala wa Kizayuni kwa ajili ya mashambulizi makubwa dhidi ya watu wa Lebanon na Gaza, imetoa wito kwa unafiki kupunguzwa mivutano na kuanzishwa amani katika eneo.

Kwa upande mmoja, Washington inadai kuunga mkono kuanzishwa usitishaji vita Gaza, na kwa upande mwingine inatoa silaha na zana za kivita zinazohitajika na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuishambulia Lebanon na kuuawa shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah na makamanda na maafisa wengi wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon na sasa Yahya al-Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas. Hivi kwa misimamo ya kinafiki kama hii, kauli za Marekani za kupigia upatu uadilifu na amani zinaweza kuaminiwa?

Suala muhimu katika muktadha huu ni onyo la wazi na la moja kwa moja la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran dhidi ya Marekani kuhusu kushirikiana na Israel katika chokochoko za kijeshi dhidi ya Iran na matokeo yake kwa Marekani katika ngazi ya kieneo.

Iran imepiga hatua kubwa katika uundaji wa makombora

 

Iran imetangaza mara chungu nzima kwamba, iwapo Marekani itashirikiana na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, kambi na suhula za kijeshi za Marekani na zana za kijeshi katika eneo hili zitakuwa shabaha halali ya mashambulizi ya Iran. Iwapo serikali ya Biden ina dhana potofu kwamba inaweza kuwa muungaji mkono wa moja kwa moja wa hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi ya mhimili wa muqawama, ikiwemo Iran, lakini isibebe gharama ya hilo, basi ipo katika makosa kabisa. Washington inapaswa kufahamu ukweli kwamba "yeyote anayepanda shari huvuna majuto".

Iran imetangaza mara kwa mara kwamba ina uwezo wa kutosha kufanya mashambulizi makali na yaliyoenea dhidi ya vikosi vya Marekani na mitambo na zana za kijeshi katika eneo hili. Hili ni suala ambalo hata vyombo vya habari vya Marekani vinalikiri. Tovuti ya The National Interest iliandika katika ripoti yake hivi karibuni kwamba: Matukio ya hivi majuzi yanaonyesha kuwa Iran ina uwezo wa kusababisha uharibifu mkubwa kwa manowari za kijeshi za Marekani na kuweka historia kwa hatua hii.

Tags