Ramaphosa aitolea wito BRICS kuwekeza pakubwa barani Afrika
(last modified Mon, 21 Oct 2024 12:05:29 GMT )
Oct 21, 2024 12:05 UTC
  • Ramaphosa aitolea wito BRICS kuwekeza pakubwa barani Afrika

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amelitolea wito kundi la BRICS kuwekeza katika maendeleo ya bara la Afrika kwa kuzingatia uwezo wa bara hilo.

Rais Cyril Ramaphosa amewasilisha ombi hilo wakati akihutubia Kongamano la Biashara la nchi wanachama wa BRICS kabla ya kufanyika Mkutano wa kundi hilo kesho Jumanne katika mji wa Kazan, Russia.  

Kiongozi wa Afrika Kusini amesema kuwa mkakati wa biashara huria wa Afrika unaanda fursa kubwa na kutoa wito kwa nchi wanachama wa BRICS kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya Afrika na weledi kwa vijana.

Mkutano wa kundi la BRICS umepangwa kufanyika Russia kuanzia tarehe 22 hadi 24 mwezi huu wa Oktoba huku wakuu wa nchi mbalimbali duniani wakitazamiwa kushiriki mkutano huo. 

Yury Ushakov Msaidizi wa Rais Vladimir Putin wa Russia ameeleza kuwa nchi 32 zimethibitisha ushiriki wao katika mkutano wa Kazan; ambapo nchi 24 zitawakilishwa na wakuu wao wa nchi na nane zilisosalia zitatuma maafisa wake wa ngazi ya juu. 

Yury Ushakov, Msaidizi wa Rais Vladimir Putin 

Si hao tu, bali wakuu wa taasisi kadhaa za kimataifa akiwemo Katibu Mkuu wa UN antonio Guterres watahudhuria mkutano huo.

Mada kuu zitakazojaliwa katika mkutano wa mjini Kazan, Russia ni pamoja na suala la ushirikiano wa kiuchumi, mikataba ya kibiashara na changamoto zinazowakabili wanachama wa BRICS, kama vile mivutano ya kijiografia, mdororo wa uchumi wa dunia na mabadiliko ya tabianchi.