Imam Khamenei: Mazungumzo na Marekani hayana maana yoyote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131184-imam_khamenei_mazungumzo_na_marekani_hayana_maana_yoyote
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amepinga ombi la Washington la mazungumzo ya nyuklia na kusema kwamba hakuna taifa lolote huru na lenye heshima linaloweza kukubali mazungumzo chini ya mashinikizo.
(last modified 2025-09-24T06:01:13+00:00 )
Sep 24, 2025 06:01 UTC
  • Imam Khamenei: Mazungumzo na Marekani hayana maana yoyote

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amepinga ombi la Washington la mazungumzo ya nyuklia na kusema kwamba hakuna taifa lolote huru na lenye heshima linaloweza kukubali mazungumzo chini ya mashinikizo.

Akihutubia taifa la Iran kwa njia ya televisheni jana usiku, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, mazungumzo na Washington chini ya mazingira ya sasa hayataleta manufaa yoyote kwa Iran na badala yake yataleta madhara makubwa ambayo hayataweza kufidiwa.

Amesema, kukubali mazungumzo chini ya mashinikizo kama hivyo kunaweza kuwa na maana kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaweza kutishwa na kulazimishwa kufanya jambo bila ya ridhaa yake.

Vilevile amesisitiza kwa kusema: kama tutafanya mazungumzo chini ya vitisho kama hivyo, itakuwa na maana kwamba tuna woga na tunaweza kusalimu amri kila tunapotishiwa kitu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kama tutakubali kufanya mazungumzo na Marekani katika mazingira haya, suala hilo halitaishia hapo. Leo, wanasema ikiwa Iran itarutubisha urani tutafanya hivi. Kesho watasema: ikiwa una makombora, tutafanya hivi... Kwa ufupi kutakuwa na vitisho visivyo na mwisho, na kutulazimisha kurudi nyuma hatua kwa hatua.

Ayatullah Khamenei aidha amesema: Wamarekani wametangaza tayari kwamba matokeo pekee ya mazungumzo lazima yawe ni kusitishwa shughuli za nyuklia za Iran na urutubishaji urani. Kwa hivyo, kama tutakaa kwenye meza ya mazungumzo na Marekani, matokeo ya mazungumzo yatakuwa yale ambayo walikuwa wameamuru huko nyuma.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amagusia pia namna Marekani inavyoshinikiza hata hivi sasa, Iran iachane na nguvu zake za makombora, si ya masafa marefu tu, bali hata ya masafa mafupi na kusema kuwa, hilo halikubaliki kabisa.