Mapigano ya kijeshi yashadidi kati ya SAF na RSF magharibi mwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131176-mapigano_ya_kijeshi_yashadidi_kati_ya_saf_na_rsf_magharibi_mwa_sudan
Mapigano ya kijeshi yameongezeka katika siku za hivi karibuni kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini huko magharibi mwa Sudan.
(last modified 2025-09-24T05:57:29+00:00 )
Sep 24, 2025 05:57 UTC
  • Mapigano ya kijeshi yashadidi kati ya SAF na RSF magharibi mwa Sudan

Mapigano ya kijeshi yameongezeka katika siku za hivi karibuni kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini huko magharibi mwa Sudan.

Wakati RSF ilidai Jumanne kwamba imechukua udhibiti wa maeneo ya kimkakati karibu na kambi kubwa ya kijeshi huko El Fasher, jeshi la Sudan lilitangaza kuzima shambulio kubwa, likithibitisha kwamba hali ndani ya mji huo imedhibitiwa kikamilifu.

Jana Jumanne vikosi vya RSF vilisambaza video kwenye mtandao wa kijamii wa X vikidai kuwa wapiganaji wake wamechukua udhibiti wa maeneo muhimu ya kijeshi karibu na makao makuu ya Idara ya Infantry ya Sita ambacho ni kituo kikuu cha jeshi huko El Fasher.

"Vikosi vyetu vinaendelea kukaza kamba kwenye maeneo hayo ya kijeshi kutoka pande kadhaa. Tunasonga mbele kwa mbinu madhubuti katika maeneo ya kaskazini, mashariki na kusini mwa mji, na pia tumeingia katika kambi ya Abu Shouk, ya watu waliokimbia makazi makazi yao," amesema mshauri wa RSF Mustafa Ibrahim.

Kwa upande wake, Jeshi la Sudan, SAF lilitangaza jana Jumanne kwamba limefanikiwa kuzima shambulio jipya la RSF kutoka upande wa kusini na kaskazini mashariki mwa El Fasher, kwa kutumia silaha mbalimbali. 

Kwa mujibu wa taarifa ya kitengo cha sita cha askari wa miguu cha SAF, mapigano hayo yaliyoanza saa kumi na mbili asubuhi kwa saa za huko, yaliongezeka na kuwa mapigano makali yaliyodumu kwa saa nane. Kimesema, jeshi la Sudan limefanikiwa "kuangamiza mamluki wa wanamgambo wa RSF" na kuwasababishia "hasara kubwa."