Amiri wa Qatar aitaja Israel kuwa ‘utawala wa kihuni’
https://parstoday.ir/sw/news/world-i131194-amiri_wa_qatar_aitaja_israel_kuwa_utawala_wa_kihuni’
Amiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, amelaani vikali vitendo vya Israel, huku akiutaja utawala huo kuwa wa "kihuni” kufuatia shambulio la karibuni lililolenga ujumbe wa mazungumzo wa Hamas mjini Doha.
(last modified 2025-09-24T12:08:01+00:00 )
Sep 24, 2025 12:08 UTC
  • Amiri wa Qatar aitaja Israel kuwa ‘utawala wa kihuni’

Amiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, amelaani vikali vitendo vya Israel, huku akiutaja utawala huo kuwa wa "kihuni” kufuatia shambulio la karibuni lililolenga ujumbe wa mazungumzo wa Hamas mjini Doha.

Shambulio hilo la “kisaliti” la Septemba 9, kama alivyoeleza kiongozi huyo wa Qatar, lilitekelezwa katika eneo la makazi linalojumuisha shule na ofisi za kidiplomasia.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa uliofanyika katika makao makuu ya UN jijini New York siku ya Jumanne, Sheikh Tamim alisema kuwa tukio hilo lilikuwa ni mauaji ya kisiasa yanayodhoofisha juhudi za kidiplomasia za kukomesha mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza.

Aliongeza kuwa: “Ukweli ni kwamba wao [Waisraeli] walikuwa wanashiriki katika mazungumzo na ujumbe huku wakipanga mauaji ya wanachama wa timu hiyo hiyo ya mazungumzo.”

Kiongozi huyo wa Qatar amebaini kuwa: “Ni vigumu mno kushirikiana na fikra isiyoheshimu hata viwango vya msingi vya diplomasia,” na kuongeza kuwa Israel huona mazungumzo kama mwendelezo wa vita, yenye lengo la kuwapotosha raia wake.

Akielezea hali mbaya Gaza, Sheikh Tamim amesema lengo la Israel ni kuifanya Gaza isiweze kukalika, kwa kuzuia upatikanaji wa elimu na huduma za afya. Alisisitiza kuwa: “Lengo lao ni kuharibu Gaza hadi isiweze kuishiwa.”

Amiri huyo alibainisha mgongano kati ya taswira ya Israel kama “eti taifa la kidemokrasia linalozungukwa na maadui” na vitendo vyake dhidi ya majirani zake, ambavyo, ni vya mauaji ya halaiki.

Sheikh Tamim amesema: “Jumuiya ya kimataifa, ikiwemo washirika wa Israel, imeanza kutambua kuwa simulizi hiyo ni kupotosha uhalisia.”

Amefananisha harakati ya mshikamano wa kimataifa na Wapalestina na upinzani wa kimataifa dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, akidokeza kuongezeka kwa uelewa na upinzani dhidi ya dhulma zilizo wazi.

Aidha, Sheikh Tamim ametoa wito wa kuheshimu utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria, akisisitiza kuwa misingi hiyo ni muhimu kwa ajili ya kudumisha amani ya dunia na heshima ya binadamu.

Akirejelea mashambulizi ya karibuni dhidi ya Qatar yaliyofanywa na Israel, amesema kuwa kuruhusu ukiukaji wa kanuni za kimataifa ni sawa na kuruhusu “utawala wa msituni,” ambapo wavamizi hutenda uhalifu bila kuadhibiwa.

Amesema amesisitiza haja ya kuheshimiana kati ya mataifa na umuhimu wa kulinda haki za binadamu na mamlaka ya kitaifa.

Mnamo Septemba 9, Israel ilitekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya makao makuu ya Hamas mjini Doha, katika operesheni ya kigaidi iliyosababisha vifo vya wanachama kadhaa wa harakati hiyo pamoja na afisa mmoja wa usalama wa Qatar.

Viongozi wa juu wa Hamas, akiwemo Khalil al-Hayya, Khaled Meshal, na Zaher Jabarin, walinusurika jaribio hilo la mauaji.

Baada ya shambulio hilo la umwagaji damu, Qatar ililaani mashambulizi hayo yaliyotekelezwa na Israel na kuyataja kuwa“ugaidi wa kitaifa,” na kuahidi kujibu mashambulizi hayo.

Qatar imeendelea kuwa mpatanishi muhimu wa kikanda katika mazungumzo kati ya Hamas na Israel.