Iran yakataa masharti ya kupunguza uwezo wa makombora yake
Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Iran amesema kuwa nchi hii itatetea kwa ari kubwa usalama wake wa kitaifa na haitakubali “masharti ya kudhalilisha” kama vile kuwekewa mipaka ya uwezo wa makombora yake, akijibu kwa ukali madai ya kupindukia kutoka mataifa ya Magharibi.
Kupitia chapisho kwenye akaunti yake ya X siku ya Jumanne, Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, amejibu kauli zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, wakati wa ziara yake katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Akizungumza akiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Rubio alidai kuwa uwezo wa makombora wa Iran ni tishio kwa mataifa ya Ghuba ya Uajemi na Ulaya.
Ikumbukwe kuwa katikati ya mwezi Juni, Israel ikianzisha vita dhidi ya Iran ambapo iliwaua kigaidi makamanda waandamizi wa kijeshi, wanasayansi, na raia wa kawaida.
Iran ilijibu uchokozi huo kwa kuvurumisha makombora ya masafa marefu na ya kasi kubwa kuelekea maeneo nyeti ya Israel ikiwemo Tel Aviv, Haifa, na miji mingine inayokaliwa kwa mabavu. Hatimaye baada ya siku 12, kupitia Marekani, utawala wa Israel ulilazimika kuomba mapigano yasitishwe.
Larijani alikuwa tayari amesema kuwa madai ya Marekani ya kutaka Iran ipunguze mpango wake wa makombora “yanapotosha mwelekeo wa mazungumzo yoyote.”
Katika chapisho lake la X, Larijani pia alizungumzia msimamo wa mataifa ya Magharibi kuhusu makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, yanayojulikana kama Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), akisema: “Marekani ndiyo iliyoondoka kwenye JCPOA, kisha Ulaya ikakiuka ahadi zake, na hatimaye wakaishambulia Iran."
Amesema: “Iran itatetea kwa ari usalama wake wa kitaifa na haitakubali masharti ya kudhalilisha hasa ya kutaka ipunguze uwezo wa makombora."
Chini ya JCPOA, Marekani na Umoja wa Ulaya walikubali kuondoa vikwazo dhidi ya Iran kwa masharti ya Iran kupunguza kiwango cha urutubishaji wa urani na kupunguza akiba yake ya nyuklia.
Makubaliano hayo yalikiukwa na Marekani wakati wa utawala wa kwanza wa Rais Donald Trump, ambaye aliondoa nchi yake kwenye mkataba huo. Licha ya hilo, Iran ilizingatia kikamilifu wajibu wake chini ya JCPOA, huku mataifa ya Ulaya pia yakishindwa kutekeleza makubaliano hayo.
Mnamo Agosti 28, Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani, kama wahusika wa JCPOA, walijulisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa wameanzisha utaratibu wa “snapback,” mchakato wa siku 30 wa kurejesha vikwazo vyote vya UN dhidi ya Iran.
Chini ya mashinikizo ya Marekani, Baraza la Usalama la UN limekataa azimio la kuondoa vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran.
Pamoja na hayo, Iran imeendelea kushiriki kidiplomasia na kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki, na imesisitiza kuwa iko tayari kufufua makubaliano ya JCPOA iwapo wahusika wengine watarejea kwenye ahadi zao.