Umoja wa Afrika na nchi za Sahel kurekebisha uhusiano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131196-umoja_wa_afrika_na_nchi_za_sahel_kurekebisha_uhusiano
Mawaziri wa mambo ya nje wa Mali, Niger, na Burkina Faso wamefanya mazungumzo na Umoja wa Afrika kuhusu kurejesha ushirikiano, ikiwemo juhudi za pamoja za kupambana na ugaidi katika nchi zao.
(last modified 2025-09-24T12:09:52+00:00 )
Sep 24, 2025 12:09 UTC
  • Umoja wa Afrika na nchi za Sahel kurekebisha uhusiano

Mawaziri wa mambo ya nje wa Mali, Niger, na Burkina Faso wamefanya mazungumzo na Umoja wa Afrika kuhusu kurejesha ushirikiano, ikiwemo juhudi za pamoja za kupambana na ugaidi katika nchi zao.

mataifa hayo matatu ya Afrika Magharibi yalikuwa yamesimamishwa uanachama katika chombo hicho cha bara Afrika kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoondoa madarakani serikali za kiraia.

Mazungumzo kati ya mawaziri wa nchi hizi tatu ambazo ni zimeunda Muungano wa Nchi za Sahel (AES) na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahmoud Ali Youssouf, yalifanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, mawaziri wa Muungano wa Nchi za Sahel wamesema: “Mkutano huu uliwezesha pande zote mbili kujadili mustakabali wa ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Muungano wa Nchi za Sahel, baada ya kipindi kilichojaa kutokuelewana na ukosefu wa mawasiliano.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, pamoja na wenzake wa Niger, Bakary Yaou Sangare, na Burkina Faso, Karamoko Jean Marie Traore, waliitaka AU kufanya maamuzi kwa kuzingatia “hali halisi” ya eneo la Sahel badala ya “kutegemea kanuni za kinadharia pekee.”

Walipongeza mpango mpya wa AU wa kutuma ujumbe wa uchunguzi katika nchi zao, wakisema hatua hiyo itasaidia kurekebisha simulizi “zisizo na msingi” zinazotolewa na “watu wasio na mawasiliano” na serikali za eneo hilo linalokabiliwa na uasi na ugaidi wenye madhara makubwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, Traore, amesema: “Hatuwezi kuzungumzia ugaidi bila Muungano wa Nchi za Sahel; hata kama tumesimamishiwa uanachama, mazungumzo kuhusu nchi zetu hayapswi kufanyika bila sisi wenyewe kuwepo.”

Mataifa hayo matatu ya Sahel yaliunda Muungano wa Nchi za Sahel mwaka jana, na kuanzisha operesheni za kijeshi za pamoja baada ya kujiondoa kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS). Walidai kuwa jumuiya hiyo ya kikanda imeshindwa kusaidia vita yao dhidi ya magaidi na kwamba inatumikia maslahi ya Ufaransa kwa gharama ya uhuru wao wa kitaifa.

Siku ya Jumatatu, maafisa kutoka makoloni ya zamani ya Ufaransa walisisitiza kuwa ugaidi unaendelea katika nchi zao “kwa sababu unaungwa mkono na baadhi ya mataifa.” Bamako, Niamey, na Ouagadougou hapo awali ziliishutumu Ufaransa na Ukraine kwa kufadhili makundi ya waasi magaidi yanayohusika na machafuko hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya AU alikiri wasiwasi wa mawaziri hao na akaahidi “kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa nchi za Muungano wa Nchi za Sahel hazitengwi” wakati wa kipindi chake cha uongozi.