Israel yathibitisha kuangamizwa kamanda wake wa Brigedi ya 401
(last modified Mon, 21 Oct 2024 07:24:35 GMT )
Oct 21, 2024 07:24 UTC
  • Israel yathibitisha kuangamizwa kamanda wake wa Brigedi ya 401

Kamanda wa Kikosi cha 401 cha jeshi la Israel ameuawa na wanamuqawama wa Palestina kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, jeshi la Israel limethibitisha.

Kwa mujibu wa jeshi la Israel, Ehsan Daqsa aliuawa baada ya kifaru chake kupigwa na mabomu katika mji wa Jabalia katika Ukanda wa Gaza jana Jumapili.

Vyombo vya habari vya Israel vimeeleza kuwa, Daqsa ni mmoja wa maafisa wakuu waliouawa katika mapigano huko Gaza. Alikuwa anatoka katika mji wa Druze eneo la Daliyat al-Karmel, na akachukua uongozi wa Brigedi ya 401 mwezi Juni.

Vyombo vya habari vya utawala huo ghasibu pia vimeripoti kuwa, makamanda wa Kikosi cha 162 na Kikosi cha 52 cha Jeshi la Israel walinaswa katika shambulio kubwa la kuvizia huko Jabalia. Ripoti za awali zinaonyesha kuwa, wanajeshi kadhaa wa Kizayuni wameangamizwa katika operesheni hiyo.

Katika hatua nyingine, afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema muqawama dhidi ya Israel uliongozwa na aliyekuwa Mkuu wa wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo, Yahya Sinwar hatimaye yatapelekea kuangamizwa utawala huo.

Khalid Mash'al, kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo nje ya nchi, aliyasema hayo mjini Istanbul, Uturuki wakati wa hafla ya maombolezo iliyofanyika kwa heshima ya Sinwar, ambaye hivi karibuni aliuawa kigaidi na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Amesisitiza kuwa, "Sinwar alianzisha dhoruba na kimbunga dhidi ya utawala wa Kizayuni na kuuadhibu kwa tetemeko kubwa la ardhi ambalo litapelekea kuangamia kwake."