Iran yakanusha kuhusika na shambulio la droni lililolenga makazi ya Netanyahu
(last modified 2024-10-20T07:03:55+00:00 )
Oct 20, 2024 07:03 UTC
  • Iran yakanusha kuhusika na shambulio la droni lililolenga makazi ya Netanyahu

Ofisi ya Uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imesema, shambulio la ndege isiyo na rubani lililolenga makazi ya Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel limefanywa na Hizbullah ya Lebanon.

Ikijibu suali kuhusu tuhuma zilizotolewa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran kwamba imehusika na shambulio la droni lililolenga makazi ya Netanyahu, ofisi hiyo imesema: "Sisi tulishatoa jibu letu hapo kabla dhidi ya Israel. Hatua hii imechukuliwa na Hizbullah ya Lebanon".

Kufuatia shambulio hilo, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni alidai "maajenti wa Iran" walidhamiria kumuua yeye na mkewe na kwamba wamefanya kosa kubwa kwa hatua yao hiyo.

Siku ya Ijumaa, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ilieleza katika taarifa kwamba, kwa kufuata miongozo ya uongozi wa Muqawama, kamandi ya operesheni za Muqawama wa Kiislamu inatangaza kuanza kwa awamu mpya na kushadidishwa makabiliano na adui Mzayuni, suala ambalo litajidhihirisha lenyewe mnamo siku zijazo.

Esmail Baghaei Hamaneh

Wakati huohuo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Esmail Baghaei Hamaneh amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel umejengwa juu ya msingi wa uwongo na upotoshaji ukweli.

Baghaei Hamaneh ametoa mjibizo huo kufuatia tuhuma mpya zilizotolewa na waziri mkuu wa utawala huo bandia kwamba maajenti wa Iran walidhamiria kumuua.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria shambulio hilo linalodaiwa kufanywa dhidi ya makazi wa Netanyahu na makelele ya propaganda yaliyofanywa na wazayuni juu ya suala hilo na akasema, utawala wa Kizayuni umejengwa juu ya msingi wa uwongo na upotoshaji ukweli na kwamba kueneza uwongo na mwenendo wa kila leo na wa kudumu wa utawala huo na vinara wake watenda jinai.../

 

Tags