Msumbiji yawaachia huru mabaharia kumi wa Kiirani
Mabaharia 10 wa Iran waliokuwa wanashikiliwa nchini Msumbiji wameachiliwa huru.
Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afrika Kusini umetangaza habari ya kuachiwa huru mabaria 10 wa Iran waliokuwa wanashikiliwa jela nchini Msumbiji.
Shirika la habari la IRNA liliandika habari hiyo jana Jumatano na kueleza kuwa, ubalozi huo ulisema kuwa mabaharia hao wa Iran walikamatwa na polisi wa Msumbiji miezi 18 iliyopita, kutokana na kuingia bila kibali katika bahari ya pwani ya nchi hiyo ya Kiafrika.
Habari zaidi zinasema kuwa, mabaharia hao wa Kiirani waliachiliwa huru na kurudishwa katika Jamhuri ya Kiislamu baada ya miezi kadhaa ya juhudi na ufuatiliaji wa kisheria, kimahakama na kisiasa.
Huko nyuma pia, mabaharia 16 Wairani waliokuwa wanashikiliwa nchini Tanzania waliachiliwa huru. Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika Eneo la Biashara Huria la Chabahar katika mkoa wa Sistan na Baluchestan kusini-mashariki mwa Iran ilisema kuwa, mabaharia hao walioachiliwa huru ni wenyeji wa mkoa wa Sistan na Baluchestan.