Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi kwa mauaji Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133102-umoja_wa_mataifa_wataka_uchunguzi_kwa_mauaji_tanzania
Umoja wa Mataifa umetowa wito wa kufanyika uchunguzi kwa kile kinachodaiwa kuwa vifo vya mamia ya watu katika machafuko ya kupinga uchaguzi nchini Tanzania.
(last modified 2025-11-12T23:06:24+00:00 )
Nov 12, 2025 23:06 UTC
  • Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi kwa mauaji Tanzania

Umoja wa Mataifa umetowa wito wa kufanyika uchunguzi kwa kile kinachodaiwa kuwa vifo vya mamia ya watu katika machafuko ya kupinga uchaguzi nchini Tanzania.

Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja huo, Volker Türk, alisema kumekuwa na jaribio la makusudi la kuficha ushahidi, kufuatia ripoti kwamba polisi walikuwa wakiichukua miili kutoka vyumba vya maiti na kuipeleka maeneo yasiyojuilikana.

Tamko la Umoja wa Mataifa lilitaja "mamia ya watu wanaaminika kuuawa" lakini umesema haujaweza kuthibitisha idadi rasmi kutokana na hali ilivyo tete nchini Tanzania, ambako huduma za intaneti zilikatwa kwa siku sita baada ya uchaguzi.

Chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kinadai kuwa watu wapatao 2,000 waliuawa kwenye siku tatu za maandamano kufuatia uchaguzi wa Oktoba 29.

Mkuu wa tume hiyo ametoa wito kwa mamlaka za Tanzania kuchunguza kwa ukamilifu na uwazi matukio haya ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, na kuwachukulia hatua waliohusika.

Kwa mara nyingine ametoa wito wa kuachiwa bila ya masharti kwa viongozi wa upinzani na wafuasi wao waliokamatwa kabla ya uchaguzi mkuu, akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye kwa mujibu wa duru za mahamakama anakabiliwa na kesi kadhaa ikiwemo ya uhaini.

Serikali ya Tanzania hadi sasa haijatoa taarifa rasmi kuhusiana na idadi ya watu waliouawa katika vurugu za uchaguzi zilizoambatana na uharibifu na uporaji wa mali za umma huku baadhi ya ripoti zikiashiria kuweko vikundi kutoka nchi za jirani vilivyoshiriki katika vurugu hizo.