Ujerumani ni muuzaji mkubwa wa pili wa silaha kwa Israel
Imeelezwa kuwa, Ujerumani inashika nafasi ya pili duniani kwa kuuuzia silaha utawala haramu wa Israel unaofanya mauaji ya kinyama dhidi ya Wapalestina.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, na sambamba na mashambulizi ya kila upande ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, Ujerumani imekuwa nchi ya pili kwa kuiuzia Israel silaha.
Kwa mujibu wa duru za Palestina, ijapokuwa Marekani imekuwa ikiupa silaha utawala wa Israel katika kipindi cha miaka miwili ya mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza, kuna nchi nyingine pia ambayo imekuwa kimya kimya katika kuupa silaha utawala wa Israel. Ripoti zinasema kuwa, Ujerumani imekuwa nchi ya pili kwa kuiuzia Israel silaha kwa wingi katika miaka hii miwili ya hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.
"Ujerumani haikuwa tu mshirika, lakini pia mwezeshaji wa mauaji ya halaiki huko Gaza," anasema Omir Bartov, mwanaharakati wa kisiasa wa Kiyahudi na mwanahistoria.
Ameongeza kuwa: "Nchi iliyowahi kusimama kidete kwa ajili ya fidia ya mauaji ya Holocaust leo hii inashiriki katika mauaji mengine ya kimbari, na utawala wa Kizayuni unaodai kuzuia maafa mengine kwa Mayahudi, umejitengenezea maafa mengine yenyewe."
Hivi karibuni gazeti la Ujerumani la Der Spiegel liliandika kuwa, zaidi ya shakhsia 200 mashuhuri wa vyombo vya habari, utamaduni na sanaa wameitaka serikali ya Ujerumani kusitisha uuzaji wa silaha kwa utawala wa Israel.