Maambukizi ya Ebola DRC yazidi kuongezeka, yapindukia visa 3,000
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140208-maambukizi_ya_ebola_drc_yazidi_kuongezeka_yapindukia_visa_3_000
Maambukizi ya virusi vya Ebola yanaendelea kuongezeka kwa kasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
(last modified 2026-07-27T09:48:28+00:00 )
Jul 27, 2026 09:47 UTC
  • Maambukizi ya Ebola DRC yazidi kuongezeka, yapindukia visa 3,000
    Maambukizi ya Ebola DRC yazidi kuongezeka, yapindukia visa 3,000

Maambukizi ya virusi vya Ebola yanaendelea kuongezeka kwa kasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Zaidi ya kesi 3,000 za maambukizi ya ugonjwa huo zimethibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku vifo vikizidi 1,260. Hali hii inajiri baada ya mamlaka za afya kuoanisha kanzidata za mikoa na zile za kitaifa, sambamba na kuripotiwa kwa makumi ya kesi mpya katika kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.

Wahudumu wa afya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamerekodi zaidi ya maambukizi 3,000 ya ugonjwa wa Ebola, vikiwemo zaidi ya vifo 1,354.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, jumla ya visa 3,075 sasa vimethibitishwa katika mikoa mitano baada ya mlipuko huo wa Ebola kuvuka maambukizi 2,000 mnamo Julai 15.

Mamlaka husika huko DRC zinasema ugunduzi wa maambukizi na juhudi za kupima zimechangia katika kugundua maambukizi zaidi.

Onyo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ni la kutisha: Mlipuko wa sasa wa virusi vya Ebola unaoenea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaweza kuwa miongoni mwa milipuko mibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani.

Katika mlipuko mbaya zaidi kurekodiwa kihistoria, ugonjwa huo wa virusi unaosababisha homa ya kutokwa damu uliua zaidi ya watu 11,000 huko Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016.

Katika mlipuko wa pili kwa ukubwa, kuanzia mwaka 2018 hadi 2020, vifo 2,287 vilirekodiwa mashariki mwa DRC.