Wananchi wa Msumbiji wapiga kura kumchagua rais na wabunge
(last modified Wed, 09 Oct 2024 10:59:15 GMT )
Oct 09, 2024 10:59 UTC
  • Wananchi wa Msumbiji wapiga kura kumchagua rais na wabunge

Raia wa Msumbiji wasiopungua milioni 17 waliojiandikisha kupiga kura mapema leo walielekea katika vituo vya kura kwa lengo la kumchagua rais mpya, wawakilishi wa bunge na magavana wa majimbo ya nchi hiyo katika uchaguzi unaotazamiwa kwa kiasi kikubwa kukibakisha madarakani chama tawala cha FRELIMO ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 49 sasa.

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji ataondoka mamlakani mwezi  Januari mwakani mwishoni mwa muhula wake wa pili wa miaka mitano.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (CNE) imesema kuwa vyama zaidi ya 36 vya kisiasa vimeshiriki katika uchaguzi wa leo. 

Wagombea wanne wameidhinishwa na Baraza la Katiba la Msumbiji kugombea kiti cha urais. Baraza hilo ni taasisi ya ngazi ya juu inayoshughulikia masuala ya kikatiba na uchaguzi.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, katika uchaguzi wa leo wa rais, Daniel Chapo, mgombea wa chama tawala Frelimo aliye na miaka 47 anakabiliana vikali na Venancio Mondlane ambaye ni mgombea binafsi. Wagombea wengine wawaili ni Ossufo Momade wa harakati ya Renamo na Lutero Simango wa chama cha Mozambique Democratic Movement (MDC).

Daniel Chapo, mgombea wa chama tawala cha Frelimo 

Huu utakuwa uchaguzi mkuu wa saba nchini Msumbiji tangu demokrasia ya vyama vingi ilipoanzishwa nchini humo mwaka 1994, miaka miwili baada ya chama cha FRELIMO kutia saini mkataba wa amani na waasi wa Renamo mjini Rome, Italia ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 16 na kusababisha vifo vya karibu watu milioni 1 na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.