Juhudi za uokoaji zinaendelea Msumbiji baada ya wiki kadhaa za mvua kubwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136032-juhudi_za_uokoaji_zinaendelea_msumbiji_baada_ya_wiki_kadhaa_za_mvua_kubwa
Juhudi za utafutaji na uokoaji zinaendelea kufanywa nchini Msumbiji baada ya wiki kadhaa za mvua kubwa iliyosababisha mafuriko makubwa, kuzamisha ardhi ya mashamba, kubomoa nyumba na miundombinu kujaa maji.
(last modified 2026-01-29T12:40:56+00:00 )
Jan 29, 2026 12:40 UTC
  • Mafuriko Msumbiji, 103 wamepoteza maisha
    Mafuriko Msumbiji, 103 wamepoteza maisha

Juhudi za utafutaji na uokoaji zinaendelea kufanywa nchini Msumbiji baada ya wiki kadhaa za mvua kubwa iliyosababisha mafuriko makubwa, kuzamisha ardhi ya mashamba, kubomoa nyumba na miundombinu kujaa maji.

Marcia Cossa, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ActionAid amesema kuna maeneo ambayo ni vigumu kufika, hasa katika jimbo la Gaza, na kwamba wanahitaji kutumia boti kwa ajili ya kufika kwenye baadhi ya maeneo kwa sababu njia ya barabara imeharibiwa na maji.

Wakati huo huo, Taasis ya Kukabiliana na Maafa na Kupunguza Hatari ya Msumbiji imeripoti kuwa watu 103 wamepoteza maisha na kwamba mafuriko makubwa yamesababisha watu wengine zaidi ya 650,000 kukosa makazi.  

Taasisi ya ActionAid imetahadharisha kuhusu hatari ya kuenea ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine ya kuambukiza katika kambi zinazowahifadhi watu zaidi ya laki moja huko Msumbiji.

Mabadiliko ya tabianchi yanayosabababishwa na binadamu yamezidisha mvua na mafuriko za hivi karibuni ambazo zimeathiri maeneo ya kusini mwa bara la Afrika na kuuwa watu zaidi ya 100. Zaidi ya wengine 300,000 wamelazimika kuwa wakimbizi. 

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Hali ya Hewa Duniani ambayo imechambua mvua mkubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko makubwa nchini Afrika Kusini na Zimbabwe umeoneysha kuwa eneo la kusini mwa Afrika lilipata mvua ya mwaka nzima katika kipindi cha siku 10. 

Nyumba na majengo mengi nchini Msumbiji yamezama kabisa, huku barabara na madaraja yakisombwa na maji katika majimbo ya  Limpopo na Mpumalanga nchini Afrika Kusini na katika baadhi ya maeneo ya Zimbabwe.

Izuddine Pinto, mtafiti mkuu wa masuala ya hali ya hewa katika Taasisi ya Hali ya Hewa ya Royal Netherlands anasema: "Utafiti wetu unaonyesha wazi kuwa, vitendo vya wanadamu vya kuendelea kuchoma mafuta ya visukuku (Fossil fuels) sio tu vinazidisha kiwango cha mvua kubwa, lakini pia husababisha matukio yenye athari mbaya na maafa makubwa."