Kipindupindu chauwa watu 12 Msumbiji huku kesi za ugonjwa huo zikiongezeka Malawi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136122-kipindupindu_chauwa_watu_12_msumbiji_huku_kesi_za_ugonjwa_huo_zikiongezeka_malawi
Msumbiji imesajili vifo vya watu 12 kutokana na ugonjwa wa kipindupindu katika muda wa saa 24 zilizopita pamoja na kesi mpya za ugonjwa huo 135. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana Jumamosi.
(last modified 2026-02-01T02:53:48+00:00 )
Feb 01, 2026 02:52 UTC
  • Kipindupindu chauwa watu 12 Msumbiji
    Kipindupindu chauwa watu 12 Msumbiji

Msumbiji imesajili vifo vya watu 12 kutokana na ugonjwa wa kipindupindu katika muda wa saa 24 zilizopita pamoja na kesi mpya za ugonjwa huo 135. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana Jumamosi.

Ripoti ya Kurugenzi ya Afya ya Umma ya Msumbiji tangu kutokea mlipuko wa karibuni nchini humo mwezi Septemba mwaka jana inaeleza kuwa kesi mpya za kipindupindu zimeongezeka katika majimbo ya Tete, Nampula na Cabo Delgado ambapo watu 12 wameaga dunia. 

Jimbo la Tete katika mkoa wa kati wa Msumbiji limekuw akitovu cha mlipuko wa kipindupindu huku idadi ya vifo ikiripotiwa kuwa zaidi ya maradufu hivi karibuni. Wakati huo huo wagonjwa 87 wapya wa kipindupindu wamesajiliwa katika jimbo hilo katika saa 24 zilizopita. 

Tarehe 28 Januari mwaka huu pekee Msumbiji ilisajili kesi mpya za kipindupindu 135 ambapo wagonjwa 49 wamelazwa hospitali kwa ajili ya matibabu. 

Mwaka jana watu 169 waliaga dunia kutokana na kipindupindu nchini Msumbiji na hivyo kuipelekea serikali ya nchi hiyo kuandaa mpango  Septemba 16 mwaka jana, kwa lengo la kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu kama "tatizo la afya ya umma" ifikapo mwaka 2030.

Innocensio Impissa msemaji wa serikali ya Msumbiji amesema kuwa lengo ni kuiona Msumbiji inasalia salama pasina na ugonjwa jwa kipindupindu kama tatizo la afya ya umma ifikapo mwaka 2030 ambapo jamii zitaweza kufikiwa na maji salama, huduma nzuri za afya n.k. 

Msumbiji imeathiriwa na mafuriko makubwa, ambayo yamesababisha vifo vya watu wengi na mamilioni ya wengine kulazimika kuhama makazi yao baada ya wiki kadhaa za mvua zinazoendelea kunyesha.