Putin: Nchi za BRICS zitachochea ukuaji wa uchumi katika miaka ijayo
(last modified 2024-10-20T11:07:23+00:00 )
Oct 20, 2024 11:07 UTC
  • Putin: Nchi za BRICS zitachochea ukuaji wa uchumi katika miaka ijayo

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa, kundi la BRICS litazalisha sehemu kubwa ya ukuaji wa uchumi wa dunia katika miaka ijayo kutokana na ukubwa wake na ukuaji wa haraka kiasi.

Alikuwa akizungumza kwenye kongamano la biashara la jumuiya hiyo siku ya Ijumaa ambalo limeitishwa kabla ya mkutano wa kilele wa BRICS utakaofanyika katika mji wa Kazan nchini Russia kuanzia tarehe 22 hadi 24 Oktoba.

Rais Putin amesema kuwa, Pato la Taifa la nchi za BRICS lilizidi dola trilioni 60 mwaka jana ikiwa ni sawa na asilimia 37.4 ya Pato la Taifa la dunia na ni zaidi ya asilimia 29.3 ya nchi za G7.

Ujumbe wake umepokewa vizuri na washiriki wa kongamano hilo ambao wanaona kuna fursa nyingi za biashara ndani ya BRICS hasa baada ya kuongezwa wanachaa 10 wa kundi hilo.

Kwa upande wake, Busi Mabuza, mwenyekiti wa Afrika Kusini ndani ya Baraza la Biashara la BRICS amesema: "Fursa kwa Afrika Kusini na kwa bara la Afrika ndani ya kundi la BRICS ni kubwa kabisa."

Alisema nchi yake ya Afrika Kusini tayari imeona ukuaji wa biashara kwa sababu ya kuwemo ndani ya BRICS.