Waasi wa M23 wadhibiti mji muhimu wa Kalembe DRC
(last modified 2024-10-22T02:23:59+00:00 )
Oct 22, 2024 02:23 UTC
  • Waasi wa M23 wadhibiti mji muhimu wa Kalembe DRC

Wapiganaji wa kundi la waasi la M23 wameuteka mji muhimu wa Kalembe wilayani Masisi na kusonga mbele hadi wilaya jirani ya Walikale mkoani kivu kaskazini katika Jamhuri ya Kiidemokrasia ya Congo.

Hatua ya waasi hao ya kudhiibiti mji huo inawapa fursa kubwa yakuviteka vijiji vyenye utajiri mkubwa wa madini wilayani Walikale.

Mji wa Kalembe unaochukuliwa kuwa njia muhimu ya kuelekea katika wilaya yenye madini ya Walikale, umekumbwa na ghasia tangu mwaka wa 2021 wakati waasi wa M23 walipoanzisha tena mashambulizi katika mkoa huo wa Kivu Kaskazini.

Wimbi la mashambulizi mapya ya waasi wa M23 na ADF linaendelea kuwatesa wananchi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na waasi wa makundi hayo mawili yakiendelea.

Wanamgambo wa ADF

 

Genge la waasi la ADF lilianzishwa katika miaka ya 1990 na makundi kadhaa ya wapinzani wa Uganda. Lilishindwa na jeshi la Uganda, lakini wanachama wake waliobakia walikimbilia maeneo ya mashariki mwa DRC na wanafanya mashambulizi ya uasi hadi hivi sasa.

Tangu mwishoni mwa 2021, wanajeshi wa Uganda na Kongo wameanzisha operesheni ya pamoja ya kupambana na waasi hao wa ADF huko mashariki mwa DRC.

Genge jingine la waasi huko mashariki mwa DRC ni lile la waasi wa M23, ambao viongozi wa DRC wanaishhutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono. Waasi hao nao kama wale wa ADF hivi sasa wameshadidisha mashambulizi yao mashariki mwa DRC na wameteka miji kadhaa tangu mwezi Juni. Wahanga wakubwa wa vitendo hivyo vya uasi ni wananchi wa kawaida hasa wanawake na watoto wadogo.