Iran yataka majirani wa Ghuba ya Uajemi wasihadaiwe na vishawishi vya Wamagharibi
(last modified 2024-10-22T02:24:53+00:00 )
Oct 22, 2024 02:24 UTC
  • Iran yataka majirani wa Ghuba ya Uajemi wasihadaiwe na vishawishi vya Wamagharibi

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran ameyataka mataifa jirani na Iran ya Ghuba ya Uajemi yasidanganyike na vishawishi vya nchi za Magharibi.

Hujjatul Islam Wal Muslimin Gholam Hossein Mohsen Ejei Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran amebainisha kuwa, tunawashauri baadhi ya majirani katika Ghuba ya Uajemi wasidanganywe na vishawishi vya baadhi ya nchi za Magharibi kuhusiana na visiwa vitatu vya Iran vya Bu Musa na Tunb Kubwa na Ndogo vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi kwa sababu watapata tabu sana.

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran ameashiria madai yasiyo na msingi yanayotolewa kila mara katika fremu ya taarifa ya kisiasa ambayo haina mashiko na kuzinasihi nchi za Ghuaba ya Uajemi kwamba, zisihadaiwe na madola ya magharibi.

 

Visiwa vya Ghuba ya Uajemi vya Abu Musa, Tunb Kubwa na Ndogo kihistoria vimekuwa sehemu ya Iran, na uthibitisho wake unaweza kupatikana na kuthibitishwa na hati nyingi za kihistoria, kisheria, na kijiografia nchini Iran na sehemu zingine za ulimwengu. Hata hivyo, Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati umekuwa ukirudia kila mara madai ya kumiliki visiwa hivyo.

Visiwa hivyo vilikuwa chini ya udhibiti wa Uingereza mwaka 1921 lakini mnamo Novemba 30, 1971, siku moja baada ya majeshi ya Uingereza kuondoka katika eneo hilo na siku mbili tu kabla ya UAE kuwa shirikisho rasmi, mamlaka ya visiwa hivyo yalirejeshwa kwa Iran.