Ghasia zaendelea kuikumba Msumbiji, miito ya utulivu yatolewa
(last modified 2024-10-22T02:22:47+00:00 )
Oct 22, 2024 02:22 UTC
  • Ghasia zaendelea kuikumba Msumbiji, miito ya utulivu yatolewa

Ghasia zilizoibuka baada ya uchaguzi nchini Msumbiji jana Jumatatu ziliendelea kuikumba nchi hiyo huku miito ya utulivu ikitolewa.

Vyombo vya usalama vya Msumbiji jana vililazimika kutumia mabomu kutoa machozi katika mji mkuu Maputo kuwatawanya waandamanaji.  Maandamano hayo sasa yamechukua sura ya kususia shughuli za serikali baada ya wito wa mgomo mkuu uliotolewa na kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane kulaani udanganyifu wakati wa uchaguzi wa rais.

Chama cha Podemos kimepinga matokeo ya uchaguzi ambayo yameonyesha kuwa chama tawala cha Msumbiji, Frelimo ambacho kimekuwa madarakani kwa nusu karne tangu uhuru,  kinaongoza.

Watu wenye silaha siku ya Jumamosi walimuua kwa risasi Elvino Dias Wakili wa Venancio Mondlane mgombea urais wa chama cha upinzani cha Podemos.

 

Paulo Guambe afisa wa chama cha Podemos pia aliuawa pamoja na Dias wakati watu waliokuwa na silaha walipoifyatulia risasi gari yao katika mji mkuu Maputo.

Raia wa Msumbiji wasiopungua milioni 17 waliojiandikisha kupiga kura tarehe 9 mwezi huu walielekea katika vituo vya kura kwa lengo la kumchagua rais mpya, wawakilishi wa bunge na magavana wa majimbo ya nchi hiyo katika uchaguzi unaotazamiwa kwa kiasi kikubwa kukibakisha madarakani chama tawala cha FRELIMO ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 49 sasa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat leo Jumatatu amelaani mauaji ya viongozi wawili wa upinzani nchini Msumbiji na kutaka uchunguzi ufanyike ili wahusika wafikishwe mbele ya sheria.