Iran na Oman zasisitiza ulazima wa kusitishwa mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na Lebanon
(last modified 2024-10-14T11:37:35+00:00 )
Oct 14, 2024 11:37 UTC
  • Iran na Oman zasisitiza ulazima wa kusitishwa mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na Lebanon

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Oman wamebadilishana mawazo kuhusu hali ya kutisha katika eneo na kutaka kusitishwa mara moja mauaji ya halaiki na uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na Lebanon.

Ismail Baqaei Hamaneh, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria katika ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake binafsi ya mtandao wa kijamii wa X, safari ya Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini Oman na kusema: 'Araghchi amekuwa na mazungumzo muhimu sana na Sayyid Badr al-Busaidi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Usultani wa Oman,  kuhusu masuala ya maslahi au wasiwasi wa pamoja.'

Msemaji wa chombo cha diplomasia cha Iran amesisitiza kuwa Araghchi na Badr al-Busaidi wamesisitiza haja ya kufanyika juhudi zaidi kwa shabaha ya kuhamasisha misaada ya kibinadamu ya kimataifa iwafikie wakimbizi wa Kipalestina.

Katika siku za hivi karibuni, Araghchi amefanya safari katika nchi za Lebanon, Syria, Saudi Arabia, Qatar na Iraq, ambapo ametangaza utayari wa Iran wa kutumia njia zote mbili za amani na vita ili kusimamisha jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza na Palestina. Ametoa ujumbe wa wazi kwa walimwengu akiwataka wafanye juhudi maradufu kwa ajili ya kusimamisha mara moja jinai hizo za utawala wa Kizayuni dhidi ya mataifa ya eneo.

Jana Jumapili Araghchi alikuwa na mazungumzo muhimu na viongozi wa ngazi za juu wa Iraq kuhusu hali tata ya usalama katika eneo hilo, na nchi mbili zikakubaliana kuongeza juhudi za pamoja, kwa ushirikiano wa nchi nyingine za eneo ili kulinda amani, utulivu na uthabiti wa eneo.

Leo asubuhi pia Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili Muscat, mji mkuu wa Oman, ikiwa ni katika sehemu ya safari zake za kieneo kwa ajili ya kufanya mashauriano ya kidiplomasia yanayolenga kuzima jinai za utawala wa Kizayuni.

Tags