Iran: HAMAS ingali hai, itaendeleza njia yake kwa nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amesema Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS iko hai na itaendelea kufuata njia yake hiyo hiyo kwa nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla licha ya kuuawa shahidi kiongozi wake Yahya Sinwar.
Araghchi ameendelea kueleza kuwa, utawala ghasibu wa Israel umeshindwa kufikia malengo yake baada ya mwaka mmoja wa vita vya mauaji ya kimbari huko Ghaza, licha ya kufanya kila uwezalo na kuua zaidi ya watu 50,000, kuharibu nyumba nyingi na kufanya jinai nyingi zinazojulikana na kila mtu.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa amefanya majadiliano ya kina na wajumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas kuhusu vita katika Ukanda wa Ghaza, mazungumzo ya kusitisha mapigano pamoja na maudhui nyinginezo.
Amesema: "Hamas iko hai zaidi kuliko wakati wowote ule" na itaendelea na mikutano yake na nchi za eneo, na akasisitiza kwamba harakati hiyo ya Muqawamna "itaendelea kufuata njia yake kwa nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla".
Katika mazungumzo hayo na Mohamed Ismail Darwish, Mkuu wa Baraza la Shura ya Hamas, Araghchi amesema, ukatili mwingi ambao Israel imeufanya huko Ghaza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita umeitia fedheha ya kudumu utawala huo ghasibu na waungaji mkono wake.
Aidha, amesema, hali mbaya ya Ghaza na Lebanon ni matokeo ya moja kwa moja ya "uungaji mkono haramu na usio na uwajibikaji" unaotolewa kwa utawala wa Israel na Marekani na madola mengine ya Magharibi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameihakikishia harakati ya Hamas kwamba damu takasifu ya kiongozi wake Sinwar, na mashahidi wengine wa Muqawama itafungua njia ya kupata uhuru kamaili kutoka kwenye makucha ya ukaliaji ardhi kwa mabavu na ukandamizaji wa Israel.../