Sisitizo la Joe Biden la kudumisha uwepo wa kijeshi wa Marekani Asia Magharibi
(last modified 2024-10-16T13:30:22+00:00 )
Oct 16, 2024 13:30 UTC
  • Sisitizo la Joe Biden la kudumisha uwepo wa kijeshi wa Marekani Asia Magharibi

White House ilitangaza siku ya Jumanne kwamba, Rais Joe Biden wa Marekani ameiandikia barua Congress ya nchi hiyo akiifahamisha kwamba vikosi vya Marekani vitaendelea kubakia katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) kwa kuhofia jibu la Iran kwa chokochoko za utawala wa Kizayuni.

Rais Joe Biden wa Marekani

Akizungumzia jibu la makombora la Tehran kwa mashambulizi ya Israel, Rais Joe Biden amesema katika barua hiyo kwamba Marekani imebadilisha muundo wa kijeshi wa nchi hiyo katika eneo kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa majeshi ya Marekani na wa utawala haramu wa Israel.

Sisitizo la rais Joe Biden la kuendelea kuwepo kijeshi Marekani katika eneo la Asia Magharibi linatimia kwa kisingizio cha kulinda kile kinachodaiwa kuwa ni kulinda maslahi ya Washington katika eneo hili nyeti, ambalo linajumuisha Ghuba ya Uajemi kama eneo la kistratijia kijiografia. Inaonekana kwamba moja ya malengo muhimu ambayo Marekani imejipangia katika eneo ni suala la kutetea na kuilinda Israel kama mshirika wake mkuu wa kistratijia.

Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, utawala habithi wa Israeli imepokea kiwango kikubwa zaidi cha msaada wa kigeni kutoka Marekani. Ripoti ya Kituo cha Utafiti cha Congress ya  Marekani inaonyesha kwamba Ikulu ya Marekani imeupa utawala huo dola bilioni 300 tangu 1948 hadi mwanzoni mwa mwaka 2023, kiasi cha fedha ambacho hata haijakitenga kwa ajili ya majimbo yake yenyewe. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba, kuusaidia utawala dhalimu wa Israel ni sheria inayopasa kufuatwa na serikali zote za Marekani, na ambayo serikali hizo zinalazimika kuitekeleza kwa ajili ya kuufanya utawala huo daima ushinde na kuwa mbele ya nchi zote za eneo kijeshi.

Kufuatia vita vya Gaza, serikali ya Rais Biden imetuma zana nyingi za kijeshi za kila aina huko Israel, silaha ambazo zinaendelea kutumiwa na utawala huo kutekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina ambapo kufikia sasa umeua shahidi zaidi ya Wapalestina 42,000 na kujeruhi wengine takriban laki moja. Mbali na msaada wa kila mwaka wa dola bilioni 3.8 kwa utawala huo katili wa Israel, Washington pia imeidhinisha mfuko wa msaada wa dola bilioni 14 kwa utawala huo dhalimu unaotenda jinai za kinyama za kila aina dhidi ya  Wapalestina  na Lebanon. Kwa mujibu wa utafiti mpya, Marekani imetoa msaada wa kijeshi wa dola bilioni 19.9 kwa Israel tangu kuanza vita vya Gaza. Ripoti hii iliyoandikwa kabla ya kuanza mashambulio ya pili ya Israel dhidi ya harakati ya Hizbullah nchini Lebanon, ni moja ya ripoti za kwanza za makadirio ya gharama za Marekani za kuisaidia Israel katika mashambulio yake huko Gaza na Lebanon.

Baada ya kufunguliwa uwanja mpya wa vita vya Israel huko Lebanon na jibu la makombora la Iran katika Operesheni ya Ahadi ya Kweli -2 ikiwa ni katika kukabiliana na ukiukaji wa utawala huo mamlaka ya Iran na ugaidi wa utawala huo, hususan mauaji ya Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas mjini Tehran,  Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na Shahidi Jenerali  Abbas Nilfuroushan, mshauri mkuu wa masuala ya kijeshi wa Iran nchini Lebanon, hivi sasa serikali ya Rais Biden inajaribu eti kuimarisha nguvu za utawala huo kwa kubakisha askari wake katika eneo na kutuma Israel mfumo mpya wa ulinzi wa anga THAAD ikidhani kuwa hilo litaweza kuudhaminia utawala huo ghasibu usalama wake. Hata hivyo uzoefu wa oparesheni ya Ahadi ya Kweli-2 ya Iran umethibitisha kwamba mifumo ya ulinzi wa anga ya utawala wa Kizayuni, hasa wa Arrow ambao ni sawa na THAAD haina uwezo wa kukabiliana na makombora ya kisasa ya balistiki ya Iran hasa lile la hypersonic la "Fattah" ambapo kulingana na ushahidi uliopo yameupa utawala huo wa kigaidi vipigo vikali vya kijeshi.  

Kombora la Iran la Fattah-2 

Suala jingine ambalo Rais Joe Biden amelitumia kama kisingizio cha kuendelea kuimarisha uwepo wa kijeshi wa Marekani Asia Magharibi ni suala la kulinda raia na mali zake dhidi ya mashambulizi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na makundi yanayofungamana nayo. Swali ni je, ni maslahi gani ambayo Marekani imejiainishia katika eneo, ambayo kwa msingi wake inakiuka sheria za kimataifa? Mfano wa wazi wa hili ni uvamizi na uwepo kinyume cha sheria wa vikosi vyake katika mikoa kadhaa ya Syria, ambao ulianza kwa kisingizio cha kupambana na magaidi wa Daesh katika kipindi cha utawala wa Barack Obama na kuendelea katika utawala wa Donald Trump na sasa katika utawala wa Joe Biden. Aidha, kuimarika uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kumefanywa kwa lengo la kuilinda Israel na kuipa kiburi cha kuendeleza uvamizi na jinai zake dhidi ya binadamu, yakiwemo mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na Lebanon na hata kuushajiisha kuongeza mashambulizi dhidi ya Syria na hatimaye kuanza kutishia kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags