Meja Jenerali Salami: Wazayuni wakifanya kosa, jibu letu litakuwa la kuumiza sana
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (SEPAH) amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel na viongozi wake wanapaswa kutambua kuwa, Operesheni ya Ahadi ya Kweli-2 lilikuwa onyo tu na kama Israel itakosea na kuthubutu kufanya uvamizi, jibu la Iran litakuwa la kuumiza sana.
Meja Jenerali Hossein Salami, kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema hayo leo katika shughuli ya mazishi ya mshauri wa kijeshi wa Iran Abbas Nilfroushan huko Lebanon na kuongeza kwamba utawala wa Israel ulidhani kimakosa kwamba kuwauwa shahidi Ismail Haniyeh, Seyed Hassan Nasrallah na Abbas Nilforoushan italeta matatizo kwa mhimili wa muqawama, lakini operesheni ya "Ahadi ya Kweli-2 kupenya kwa makombora ya Iran katika ngao ya chuma ya utawala wa Kizayuni ni mambo ambayo yalivuruga mlinganyo huo.
Meja Jenerali Salami alifafanua kwamba dhana ya kuwa mapambano ya muqawama yatakoma kwa kuuawa shahidi viongozi na majenerali si kitu chochote zaidi ya kuwa njozi tu, kama vile baada ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH), uimara na mamlaka ya harakati ya upinzani iliongezeka.
Shahid Nilforoushan aliuawa kikatili tarehe 27 Septemba 2024, kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon akiwa pamoja na Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchi hiyo.
Shahid Nilforoushan alikuwa mmoja wa shakhsia na makamanda muhimu sana wa Iran aliyeongoza operesheni nyingi za kuwasaidia Walebanon na Wapalestina katika kupambana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.