Oct 06, 2024 07:27 UTC
  •  Ismail Baqaei
    Ismail Baqaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Uingereza huko Sana'a, Al Hudaydah na maeneo mengine ya Yemen.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Ismail Baqaei, amesema kuwa, mashambulizi ya mara kwa mara ya kijeshi za Marekani na Uingereza huko Yemen ni ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na misingi mikuu ya sheria za kimataifa.

Baqaei amesema, sababu kuu ya kuendelea ukosefu wa usalama na amani katika eneo hili la Magharibi mwa Asia ni kuendelea uvamizi na sera za vita na kutaka kujipanua za utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesisitiza udharura wa kukomeshwa uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Lebanon na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo katika Ukanda wa Gaza, kama sharti la kurejeshwa amani na utulivu katika eneo hilo.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amefafanua kuwa, hatua za wananchi wa Yemen na mataifa mengine ya Kiislamu za kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina, Lebanon na Syria ni jibu la kimaumbile dhidi ya mauaji ya ndugu zao wa Kipalestina na Lebanon.

Ndege za kivita za Marekani na Uingereza zinashambulia maeneo mbalimbali ya Yemen

Ismail Baqaei amesema, ni dhahiri kuwa, utumiaji haramu wa nguvu za kijeshi unaofanywa na Marekani na waitifaki wake dhidi ya taifa makini la Yemen hautakuwa na taathira yoyote katika azma yao ya kuwatetea watu wa Palestina na Lebanon. 

Ndege za kivita za Marekani na Uingereza mapema jana Jumamosi zilishambulia mara tatu eneo la "Al Jabbanah" kaskazini-magharibi mwa mji wa Al Hudaydah, huko magharibi mwa Yemen.

Tags