Duru za Israel: Hizbullah imeshajijenga upya, sasa tusubiri vita
Mashirika ya usalama ya Israel yametangaza kwamba yanajiandaa kwa ajili ya kuingia kwenye vita vikubwa na Hizbullah ya Lebanon yakidai kuwa harakati hiyo imeshajijenga upya kijeshi na sasa lazima wasubiri majibu makali kutoka kwa harakati hiyo.
Kanali ya 11 ya televisheni ya Israel iliripoti jioni ya jana Jumatatu ikiyanukuu mashirika ya kijasusi ya Israel yakidai kuwa Hizbullah imeshajijenga upya kisilaha na kwa mbinu za kijeshi na kisiasa katika maeneo ya kaskazini mwa Mto Litani na karibu na Beirut.
Utawala wa Kizayuni umedai pia kwamba serikali ya Lebanon imeonesha udhaifu mkubwa mbele ya nguvu inayoongezeka ya Hizbullah na kutishia kuanzisha mashambulizi dhidi ya Lebanon.
Duru hizo za usalama za Israel zimedai kuwa utawala wa Kizayuni haushambulii mji mkuu Beirut kwa hofu ya kuzusha vita vikubwa. Zimekiri kwamba mashinikizo ya Marekani na Wazayuni yameshindwa kuzuia kujijenga upya Hizbullah.
Jeshi la Israel limekuwa likizidisha mashambulizi yake ya anga karibu kila siku ndani ya Lebanon kwa wiki kadhaa sasa. Israel imeshaua zaidi ya watu 4,000 tangu ilipoanza mashambulizi yake ya ardhini huko Lebanon mwezi Oktoba 2023.
Utawala huo unaendelea kukanyaga makubaliano ya kusitisha mapigano na Hizbullah, ambayo yalianza kutekelezwa mwezi Novemba 2024. Umeshakanyaga makubaliano hayo kwa zaidi ya mara 4,500.
Kanali ya 11 ya televisheni ya Israel imedai kwamba, maafisa wa Israel na Marekani wamekatishwa tamaa na serikali ya Lebanon kutokana na kushindwa kuipokonya silaha Hizbullah na kwamba hivi sasa harakati hiyo imesharejesha nguvu zake na iko tayari kuingia vitani ni Wazayuni.