Mama Samia aapishwa kwa muhula mwingine wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132758-mama_samia_aapishwa_kwa_muhula_mwingine_wa_urais
Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameapishwa leo Jumatatu kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mpya wa miaka mitano. Rais Samia ameapishwa baada ya uchaguzi uliogubikwa na vurugu.
(last modified 2025-11-04T06:22:36+00:00 )
Nov 03, 2025 11:35 UTC
  • Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameapishwa leo Jumatatu kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mpya wa miaka mitano.
    Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameapishwa leo Jumatatu kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mpya wa miaka mitano.

Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameapishwa leo Jumatatu kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mpya wa miaka mitano. Rais Samia ameapishwa baada ya uchaguzi uliogubikwa na vurugu.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameapishwa kwa muhula wa pili chini ya ulinzi mkali, kufuatia uchaguzi uliokumbwa na ghasia na kupingwa na upinzani.

Hafla ya kuapishwa kwake imefanyika katika uwanja wa kijeshi katika mji mkuu wa Dodoma.

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania huu ni muhula wa pili wa Rais Samia japokuwa ameongoza kwa miaka minne baada ya kumrithi mtangulizi wake Hayati John Magufuli.

Hafla ya kuapishwa Rais Samia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Marais wa Zambia, Somalia na Burundi, Makamu wa Rais wa Uganda na Kenya, Pamoja na mabalozi na wanadiplomasia mbalimbali.

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa, Rais Samia Suluhu Hassan amewashukuru wanasiasa walioshiriki uchaguzi wakiwemo wagombea wengine 16 waliowania kiti cha urais.

Amesema wanasiasa hao wametambua kuwa "uchaguzi sio vita". Kiongozi huyo pia amewapongeza wale waliochaguliwa kushika nafasi za ubunge na udiwani kote nchini humo na kuwahimiza kujielekeza kuchapa kazi kwa ajili ya raia wa taifa hilo.

Aidha akihutubia baada ya kuapishwa Rais Samia Suluhu Hassan amewashukuru wapiga kura waliompa ridhaa ya kuongoza na akatoa mwito wa kusahau yaliyopita hasa matukio ya baada ya uchaguzi na kudumisha umoja na mshikamano kwa ajili ya kujenga nchi.

Aidha amesema atafanya kila jitihada kuliunganisha taifa la Tanzania na kuonya kuhusiana na madhara na machafuko na vurugu ambazo amesema hazina faida kwa mtu yoyote.

Katika hotuba yake katika hafla ya kuapishwa Rais wa Tanzania, Rais Hakainde Hichilema wa Zambia amemtolea mwito Rais Samia Suluhu Hassan kunyoosha mkono wa mapatano na upinzani na wale wanaopinga utawala wake au hakumchagua katika uchaguzi uliomalizika.

Kwa upande wake Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi akihutuubia katika hafla hiyo amepongeza Tanzania kwa kumaliza uchaguzi.

Amesema; "Ningependa kuwapongeza ninyi raia wote wa Tanzania kwa namna mlivyopiga kura... katika ulimwengu wa leo, kwa wananchi, upigaji kura ni kama mtihani, mmefaulu mtihani, hongereni sana... Amani haina bei na watanzania mmeelewa vizuri msemo huo."