Mapitio ya jinai za Magharibi; jinai za Marekani nchini Somalia
-
Marekani imefanya mashambulizi ya anga na operesheni za kijeshi nchini Somalia.
Marekani imefanya mashambulizi ya anga na operesheni za kijeshi nchini Somalia, na kusababisha vifo vingi vya raia, na akthari ya hatua hizo zimekuwa zikikosolewa na makundi ya kutetea haki za binadamu. Idadi halisi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko ile iliyotangazwa na Pentagon.
Uingiliaji wa kijeshi wa Marekani nchini Somalia ni sehemu ya kile kinachoitwa vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi kufuatia tukio la Septemba 11. Uingiliaji kati huu umekuwa ukiendelea tangu 2007 na umejumuisha operesheni za anga, usaidizi wa kijasusi, mafunzo kwa vikosi vya ndani, na ushirikiano na vikosi vya Umoja wa Afrika.
Licha ya madai ya Marekani ya kulenga makundi ya kigaidi kama vile Al-Shabaab na Daesh, ripoti nyingi zinaonyesha kwamba, mashambulizi haya mara nyingi husababisha vifo vya raia, na mwingi wa ukatili huu bado umefichwa na vyombo vya habari vya Magharibi. Kwa mfano, katika Vita vya Mogadishu mnamo Oktoba 1993, mamia ya Wasomali waliuawa na majeshi ya Marekani.
Mashambulio ya ndege zisizo na rubani
Mojawapo ya vipengele muhimu zaidi vya uingiliaji kati huu kimekuwa ni mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za jeshi la Marekani, yaliyofanywa kwa kutumia ndege zisizo na rubani za MQ-9 Reaper. Mashambulizi haya yamefanyika hasa katikati na kusini mwa Somalia, kwa lengo la kuwaondoa wanachama wa makundi ya wanamgambo.
Hata hivyo, ripoti kutoka za mashirika ya kimataifa zinaonyesha kwamba, idadi halisi ya raia majeruhi ni hadi mara 30 zaidi ya takwimu rasmi za Pentagon. Kwa mfano, katika shambulio katika mji wa Beledweyne, Pentagon ilidai kuwa ni wanachama 13 pekee wa Al-Shabab waliouawa na hakuna raia aliyejeruhiwa. Lakini vyanzo huru viliripoti kuwa zaidi ya raia 20 waliuawa.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika lisilo la kiserikali la Airwars linalofuatilia mashambulizi ya anga ya kimataifa, jeshi la Marekani limefanya operesheni 260 nchini Somalia kuanzia 2007 hadi mwisho wa Agosti 2022.
Pentagon, sambamba na kuthibitisha idadi hii ya operesheni, inadai kuwa raia watano wameuawa na 11 wamejeruhiwa tangu wakati huo. Wakati huo huo, Taasisi ya Airwars inakadiria kuwa takriban raia 78 hadi 153, wakiwemo watoto 20 hadi 23, wamepoteza maisha katika mashambulizi yaliyothibitishwa na Pentagon.
Matokeo ya kiuchumi na kijamii
Taasisi ya Airwars imesema kuwa, mashambulio ya mabomu nchini Somalia yaliyofanywa na jeshi la Marekani sio tu kwamba hayajasaidia kuimarisha usalama wa eneo hilo, bali yamepelekea kuendelea ukosefu wa utulivu na umaskini ulioenea miongoni mwa watu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Mbali na roho za watu kupotea, mashambulizi hayo yameshadidisha ukosefu wa utulivu zaidi nchini Somalia.
Katika hali ambayo, Marekani inadai kuisaidia serikali ya shirikisho ya Somalia kwa hatua hizi, wachambuzi wengi wanaamini kuwa, kuwepo kwa jeshi la kigeni, hasa bila ya uangalizi wa kimataifa, kumezidisha ghasia na kuimarisha makundi yenye misimamo ya kufurut ada.
Kundi la Al-Shabaab, mshirika wa mtandao wa al-Qaeda, limetumia mashambulizi hayo kusajili na kueneza propaganda dhidi ya Magharibi, na limeweza kuongeza ushawishi wake katika baadhi ya maeneo.
Trump na Somalia
Kwa kuchaguliwa tena Donald Trump, mashambulizi ya anga ya Marekani nchini Somalia yalifanyika kwa madai ya kuwalenga wanachama wa Daesh, lakini ripoti huru zinaonyesha majeruhi ya raia ambayo yamefichwa katika taarifa rasmi. Kwa mfano, katika siku za kwanza za muhula wa pili wa Trump, jeshi la Marekani lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya maeneo ya kundi la kigaidi la Daesh nchini Somalia.
Trump alidai kwenye mitandao ya kijamii kwamba mashambulio hayo yalikuwa makini na yalifanyika "bila madhara hata kidogo kwa raia." Hata hivyo, makundi ya haki za binadamu na vyanzo vya ndani yamewasilisha simulizi tofauti na hiyo. Mashuhuda wameripoti vifo vya raia kadhaa wakiwemo wanawake na watoto wakati wa mashambulio ya mabomu kwenye mapango na maeneo jirani.
Migongano hii ya maelezo rasmi na ripoti huru imeibua wasiwasi kuhusu uwazi na uwajibikaji wa jeshi la Marekani. Kwa ujumla, mashambulizi ya Marekani nchini Somalia wakati wa muhula wa pili wa rais Trump, licha ya kudai kuwa anapambana na ugaidi, lakini yamesababisha hasara zaidi na kutoaminiana miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Mukhtasari
Uingiliaji kati wa Marekani nchini Somalia sio tu kwamba umeshindwa kupunguza ugaidi, lakini pia umeongeza vifo vya raia, umma kutokuwa na imani na serikali kuu, na kuimarika kwa makundi yenye misimamo ya kuchupa mipaka. Mashirika ya haki za binadamu yametaka kuwepo kwa uwazi kuhusu mashambulizi haya na maafisa wa Marekani kuwajibika.
Pia, wanaharakati wengi wa haki za binadamu wanasisitiza kuwa, matumizi ya nguvu bila ya uangalizi wa kimataifa na bila kuzingatia madhara ya kibinadamu ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na sheria za kimataifa.
Hali hii inaonesha kuwa, sera za uingiliaji kati za Marekani katika nchi dhaifu na zilizokumbwa na migogoro si tu kwamba si suluhu, bali nazo ni sehemu ya tatizo. Somalia, nchi ambayo imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na umaskini kwa miaka mingi, sasa inakabiliwa na changamoto mpya, baadhi zikiwa ni matokeo ya moja kwa moja ya hatua za kijeshi za Marekani.