Araghchi: Marekani itapata majuto makubwa kwa kuizamisha manowari ya Iran ya Dena
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi ametoa mjibizo kwa hatua ya jeshi la kigaidi la Marekani ya kuilenga na kuigharikisha manowari ndogo ya Dena na kusisitiza kwamba, Washington itapata majuto makubwa kwa kuanzisha mwenendo huo.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X leo Alkhamisi, Araghchi ameandika: Marekani imesababisha janga jengine ambalo mara hii ni la baharini na katika masafa ya maili elfu mbili kutoka pwani ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, manowari ya Dena, ambayo ilikuwa mgeni wa Jeshi la Wanamaji la India ikiwa imebeba mabaharia wapatao 130, imelengwa katika maji ya kimataifa pasi na kupewa tahadhari yoyote; na kwa sababu hiyo amesisitiza kwa kusema: “mtaona; Marekani itapata majuto makubwa”.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, manowari ya mashambulizi ya Dena, ambayo ilikuwa ikirudi nchini kutoka kwenye mazoezi ya pamoja ya majini na India, imeshambuliwa na kuzamishwa na nyambizi ya Marekani ikiwa katika pwani ya Sri Lanka.
Zaidi ya mabaharia 80 wa manowari hiyo wameuawa shahidi katika hujuma hiyo ya kigaidi…/