Military Watch: Fattah 2 haiwezi kuzuiwa na makombora ya Marekani
-
kombora jipya la hypersonic la Iran, Fattah 2
Jarida maarufu la Military Watch limefichua kuwa ni karibu muhali kuweza kuzuia kombora jipya la hypersonic la Iran, Fattah 2, kutokana na kasi yake ya kustaajabisha na uwezo wake mkubwa wa manuva.
Ni baada ya kutangaza kuwa, Iran imeanza kutumia makombora yake ya hypersonic ya Fattah 2 dhidi ya shabaha za Marekani na Israel.
Jarida hilo la utafiti wa masuala ya kijeshi limechapicha picha ya mashambulizi ya karibuni ya Iran dhidi ya maeneo muhimu ya Israel na kusema kuwa, teknolojia ya kisasa iliyotumiwa katika kombora la Fattah 2 ni hatua muhimu sana katika mlingano wa kijeshi wa Asia Magharibi.
Jarida hilo limeripoti kuwa utumiaji wa makombora hayo ni dhihirisho la uwezo wa aina yake na ishara ya kuongezeka upeo wa mapigano ya sasa.
Ripoti ya uchambuzi ya Military Watch imesisitiza kuwa, kuingia Iran katika klabu ya nchi zenye makombora ya hypersonic kunatoa changamoto kubwa kwa mifumo ya ulinzi wa anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Military Watch imeripoti kuwa kombora hilo lenye uwezo wa kulenga shabaha umbali wa kilomita 1400 lina kichwa cha mlipuko chenye kasi kubwa ya Mach 13 hadi 15 (karibu kilomita 18,500 kwa saa). Jarida hilo limeripoti kuwa kasi na uwezo wa manuva wa kombora hilo la Fattah 2 unafanya kazi ya kuweza kuliwinda kuwa muhali.
Military Watch imesema utumiaji wa makombora mapya ya Iran katika vita vya sasa umetatiza sana mipango ya Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel.