Majasusi watano wa Israel watiwa mbaroni Ghaza
Kikosi cha kujihami kiitwacho "Rad'e" kinachoshirikiana na Muqawama kwa ajili ya kulinda usalama huko Ghaza, jana Jumatatu kilifanya operesheni ya kiusalama kusini mwa mji wa Khan Yunis na kuwatia mbaroni majasusi watano wa Israel.
Duru za Palestina zimeripoti kwamba wakati wa operesheni hiyo, mamluki 5 wa "Hussam Al-Astal" wametiwa mbaroni baada ya kutiliwashaka, kufuatiliwa shughuli zao na kugundulika kuwa ni majasusi wa Israel.
Askari wa kikosi cha Rad'e wameripoti kwamba wamefanikiwa pia kukamata silaha na pesa kutoka kwa majasusi hao ambazo zilikuwa zinatumika kufadhili vitendo vya kihalifu. Lengo la njama zote hizo za Wazayuni ni kudhoofisha Muqawama wa wananchi wa Ghaza na kuvuruga mshikamano wa wananchi hao.
Kikosi cha Rad'e kimesisitiza kuwa kitaendelea kuwafuatilia kwa nguvu zote mamluki na majasusi wa Israel na kusambaratisha mitandao yao yote.
Kikosi hicho cha kulinda usalama wa Ghaza kimebainisha pia kuwa Muqawama unafanya kila uwezalo kudumisha usalama wa umma na utulivu katika shughuli zao.
Hussam Al-Astal alikuwa afisa wa zamani wa usalama wa Palestina ambaye alishtakiwa kwa kuwa jasusi wa Israel katika miaka ya 1990.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022 ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ghaza, Al-Astal ilihusika katika mauaji ya mwanasayansi wa Palestina Fadi al-Batsh nchini Malaysia mwaka 2018.
Jasusi huyo alikiri kushiriki katika operesheni hiyo kwa amri ya shirika la kijasusi la Israel Mossad. Mahakama ya kijeshi ya Ghaza ilimuhusisha Al-Astal na mauaji hayo na kutoa hukumu ya kifo kwa wale walioshiriki katika uhalifu huo.