Yemen: Tumejiandaa kwa vita vikubwa na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i132808-yemen_tumejiandaa_kwa_vita_vikubwa_na_israel
Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, harakati za Muqawamaa zimejiandaa kwa ajili ya awamu ijayo ya mapambano na utawala wa Kizayuni wa Israel, kwani zinaamini kwamba eneo hili halitakuwa imara kwa muda mrefu maadamu Palestina inaendelea kukaliwa kwa maabavu na dola pandikizi la Kizayuni ambalo muda wote linapanga njama dhidi ya Waislamu.
(last modified 2025-11-05T05:46:17+00:00 )
Nov 05, 2025 03:17 UTC
  • Sayyid Abdul Malik al Houthi, Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen
    Sayyid Abdul Malik al Houthi, Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen

Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, harakati za Muqawamaa zimejiandaa kwa ajili ya awamu ijayo ya mapambano na utawala wa Kizayuni wa Israel, kwani zinaamini kwamba eneo hili halitakuwa imara kwa muda mrefu maadamu Palestina inaendelea kukaliwa kwa maabavu na dola pandikizi la Kizayuni ambalo muda wote linapanga njama dhidi ya Waislamu.

Sayyid Abdul Malik al Houthi amesema hayo katika hotuba iliyorushwa hewani jana Jumanne wakati wa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Mashahidi na kusisitiza kuwa, baada ya awamu ya kwanza ya mapambano na Wazayuni, wananchi wa Yemen wamepata nguvu kubwa zaidi kuliko huko nyuma.

Amezungumzia operesheni za majini na angani zilizofanywa na vikosi vya Yemen kwa miezi kadhaa dhidi ya Israel ili kuulazimisha utawala wa Kizayuni kukomesha jinai na mauaji yake ya umati huko Ghaza na kusema kuwa, hata wakati Israel na washirika wake yaani Marekani na Uingereza na madola vibaraka ya kieneo na kimataifa yalipoanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen, taifa hilo la Kiarabu liliendelea kuwa imara na mashambulizi yake ya angani na baharini dhidi ya Israel yaliendelea.

Katika sehemu moja ya hotuba yake, Sayyid Abdul Malik al Houthi amesema: "Hakika tunaelekea kwenye duru nyingine ya mapambano na adui Israel. Eneo letu hili haliwezi kuwa na utulivu, usalama na amani maadamu Israel inaendelea kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Palestina na inaendelea na njama zake dhidi yetu kama umma wa Kiislamu."

Vilevile amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa watu wa Yemen heshima kutokana na msimamo wao imara wa kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina na kutokana na Yemen kuisaidia Ghaza katika vita vyake na Wazayuni hadi pale Israel ilipolazimika kutia saini makubaliano ya kusimamisha vita.