Waasi wa M23 wauteka mji wa Walikale mashariki mwa Kongo DR
(last modified Fri, 21 Mar 2025 03:23:20 GMT )
Mar 21, 2025 03:23 UTC
  • Waasi wa M23 wauteka mji wa Walikale mashariki mwa Kongo DR

Kundi la waasi la M23, linaloendesha mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, limeuteka mji wa Walikale unaopatikana katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini huko Kivu Kaskazini.

Radio Okapi ya ncini Kongo imetangaza kuwa waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na jeshi la Rwanda wameuteka mji huo bila ya kujiri mapigano. 

Hatua hii imejiri baada ya Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kutoa wito wa kusitishwa mapigano na uhasama mara moja, na bila masharti, wakati wa mazungumzo yao mjini Doha, Qatar.

Duru za habari ndani ya Kongo zimeeleza kuwa mji wa Walikale ambao una akiba kubwa ya madini ya bati siku kadhaa zilizopita ulikuwa ukitishiwa na waasi ambao walikabiliana vikali na vikosi vya serikali ya Kinshasa huku jeshi la Kongo likisaidiwa na kundi la wanamgambo lenye mfungamano na jeshi la Kongo kwa jina la "Wazalendo." Mapigano hayo yalijiri katika vitongoji vya mji wa Walikale na kupelekea raia kukimbilia katika maeneo salama. 

Waasi wa M23 wameshadidisha mashambulizi na hujuma zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwezi Disemba mwaka jana na kufanikiwa kuuteka mji wa Goma na makao makuu ya jimbo la Bukavu. 

Mapema mwezi huu wa Machi, waasi hao waliuteka mji wa Nyabiondo unaopatikana kilomia 110 kaskazini magharibi mwa mji wa Goma katika jimbo la Kivu ya Kaskazinini baada ya mapigano makali ya siku kadhaa kati yao na vikosi vya serikali na wanamgambo wenye mfungamano na serikali ya Kinshasa. 

Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa mzozo wa mashariki mwa Kongo umepelekea maelfu ya raia wa nchi hiyo kukimbilia katika maeneo na nchi jirani ili kukwepa mapigano.