Al-Jazeera: Israel inajiandaa kuanzisha tena mashambulizi makali Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135044-al_jazeera_israel_inajiandaa_kuanzisha_tena_mashambulizi_makali_gaza
Waziri wa Vita wa Israel, Israel Katz ameliagiza jeshi la utawala huo haramu kujiandaa kurejea kwenye mapigano makali dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas katika Ukanda wa Gaza, hayo yameripotiwa na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ikinukuu gazeti la Kizayuni la The Jerusalem Post.
(last modified 2026-01-03T02:37:55+00:00 )
Jan 03, 2026 02:37 UTC
  • Al-Jazeera: Israel inajiandaa kuanzisha tena mashambulizi makali Gaza

Waziri wa Vita wa Israel, Israel Katz ameliagiza jeshi la utawala huo haramu kujiandaa kurejea kwenye mapigano makali dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas katika Ukanda wa Gaza, hayo yameripotiwa na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ikinukuu gazeti la Kizayuni la The Jerusalem Post.

Kwa mujibu wa chanzo cha usalama kilichonukuliwa na The Jerusalem Post, kuna uwezekano mdogo tu kwamba Israel itaruhusu bidhaa kuingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah kwenye mazingira ya sasa. Chanzo hicho kimesema kuruhusu bidhaa muhimu kuingia Gaza kwa wingi kutawezesha ujenzi mpya wa eneo hilo bila 'matakwa muhimu' ya Israel kutimizwa.

Miongoni mwa matakwa hayo ni pamoja na kurejeshwa kwa mabaki ya Sajenti Mkuu Meja Ran Gvili, aliyeelezwa kama mateka wa mwisho wa Israel, pamoja na kuondolewa kwa wanajeshi katika Ukanda wa Gaza na kupokonywa silaha Hamas.

Israel inaendelea kukiuka mapatano ya kusitisha vita iliyofikia kati yake na Hamas. Aidha utawala huo pandikizi umesema hautaondoka Gaza na kwamba itaanzisha eneo pana kwa jina la "Buffer Zone" katika ukanda huo, licha ya kukiwa kuondoka kikamilifu Gaza kwa mujibu wa mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusimamisha vita wenye vipengee 20.

Hii ni katika hali ambayo, Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina imeripoti kuwa, mwaka uliomalizika wa 2025 ulikuwa mwaka mbaya zaidi katika uga wa kibinadamu na idadi ya jamii ya watu huko Palstina kutokana na vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kuongezeka kwa ukiukaji wa sheria katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, Wapalestina zaidi ya 72,000 wameuawa shahidi tangu kuanza vita na mauaji ya kimbari ya Israel Oktoba 7, 2023 ambapo asilimia 98 ya vifo vimesajiliwa huko Gaza. Kiwango hicho kimetajwa kuwa kikubwa sana kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina.