Kusimama kidete Somalia dhidi ya mpango hatari wa Wazayuni huko Somaliland
-
Mohamed Omar, Waziri Mshauri katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Somalia
Somalia imeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu kuwahamisha kwa lazima wa Wapalestina na kuwapeleka Somaliland ambalo limejitangazia uhuru.
Mohamed Omar, Waziri Mshauri katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Somalia, amesema kwamba utawala wa Kizayuni unatafuta kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza hadi eneo la "Somaliland" na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati mara moja ili kuzuia utekelezaji wa mpango huo wa Tel Aviv.
Mohamed Omar amesisitiza ulazima wa Tel Aviv kuheshimu umoja wa ardhi ya Somalia, na akasema kwamba nchi yake haitazungumza na upande wowote ambao unakiuka uhuru na mamlaka yake ya kitaifa na umoja wa ardhi yake.
Afisa huyo wa Somalia amebainisha kuwa kutambua eneo lililojitenga la Somaliland hakutakuwa na msaada wowote kwa amani, bali kutazidisha ukosefu wa utulivu katika eneo hilo, na kwamba Mogadishu katu haitakuwa tayari kufanya mazungumzo chini ya mashinikizo. Omar ameuonya utawala wa Kizayuni, dhidi ya kuanzisha kambi ya kijeshi huko Somaliland.
Kadhalika katika Kongamano la 17 la Aljazeera huko Qatar, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Muhamud, akizungumzia umuhimu wa kimkakati wa Bahari Nyekundu kama njia muhimu ya biashara ya kimataifa, alionya kwamba tishio lolote kwa utulivu wa njia hii ya baharini litakuwa na matokeo mabaya kwa uchumi wa dunia. Katika muktadha huo huo, alionya dhidi ya hatua haramu ya utawala wa Kizayuni ya kuitambua Somaliland akisema kwamba, hatua hiyo inakiuka uhuru na umoja wa ardhi ya Somalia na bila shaka ni tishio kubwa kwa utulivu wa eneo la Pembe ya Afrika na Bahari Nyekundu.
Hatua za serikali ya Somalia za kukabiliana na kujitenga Somaliland zinafuatiliwa ndani ya mfumo wa malengo ya kisiasa, usalama na uhuru. Somaliland ilitangaza uhuru wake kwa upande mmoja tangu 1991, lakini hadi sasa hakuna serikali iliyoitambua. Hii ni katika hali ambayo Desemba mwaka jana (20250 utawala wa kibaguzi wa Israel ulitangaza kulitambua rasmi eneo la Somaliland kama nchi huru hatua ambayo imefanyika katika fremu ya malengo yake ya kujitanua duniani. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na ongezeko la ushindani wa kikanda katika Pembe ya Afrika na kuingia madola ya kigeni katika eneo hilo, suala la Somaliland limekuwa nyeti zaidi kwa Mogadishu, na serikali kuu imejaribu kuzuia kuimarika mchakato wa kujitenga ikitumia njia za kidiplomasia, kisheria na kiusalama. Kuhusiana na hilo, Somalia inafuatilia malengo kadhaa:
Lengo la kwanza la Somalia ni kuimarisha umoja wa ardhi yake na kuzuia mfano hatari kuwekwa katika eneo hilo. Serikali ya Mogadishu ina wasiwasi kwamba kutambuliwa Somaliland rasmi au kwa njia isiyo rasmi na baadhi ya watendaji wa nje, hasa katika muktadha wa mikataba ya kiuchumi au usalama, kunaweza kudhoofisha msimamo wa serikali kuu na kuhimiza maeneo mengine kufuata mfano huo. Kwa hivyo Somalia inajaribu kuzuia Somaliland kupata uhalali kwa kuongeza harakati za kidiplomasia, ikionya kuhusu matokeo ya kisheria ya kujitenga, na kutafuta msaada kutoka Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Lengo la pili ni kuzuia ushawishi wa mataifa ya kigeni katika eneo lenye umuhimu mkubwa wa kijiografia. Pembe ya Afrika imekuwa uwanja wa ushindani kwa nchi mbalimbali katika miaka ya hivi karibuni, na Somalia ina wasiwasi kwamba maingiliano ya moja kwa moja kati ya baadhi ya serikali, hasa utawala wa Israel, na Somaliland, hasa katika maeneo ya bandari na kijeshi, yatasababisha nyufa kubwa zaidi katika muundo wa nchi. Hatua mpya za Somalia bila shaka ni jaribio la kudhibiti mchakato huu na kuzuia Somaliland kuwa kitovu cha watendaji wa kigeni.
Lengo la tatu ni kuimarisha mshikamano wa ndani na kutuma ujumbe wa wazi na imara kwa makundi ya kieneo. Kwa kuchukua msimamo mkali na amilifu zaidi kuhusu Somaliland, serikali ya Somalia inajaribu kuonyesha uwezo wake wa kutumia uhuru na kudhibiti migogoro ya ndani. Hatua hizi pia ni sehemu ya juhudi pana za kujenga upya serikali, kuimarisha taasisi za usalama, na kuongeza imani ya umma kwa serikali kuu.