Oct 05, 2024 06:15 UTC
  • Balozi wa Marekani Uganda atakiwa aombe msamaha au afukuzwe nchini

Mkuu wa Jeshi la Uganda Jeneral Muhoozi Kainerugaba amemtaka balozi wa Marekani nchini humo William Popp amuombe msamaha Rais Yoweri Museveni au atimuliwe nchini.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa kijamii wa X, Jenerali Muhoozi  amesema sababu ya kumtaka balozi huyo aombe radhi ni kutokana na hatua yake ya kumvunjia heshima rais sambamba na kuidharau katiba ya Uganda.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, Mkuu wa Jeshi la Uganda alisema iwapo balozi wa Marekani hatamuomba msamaha Rais Museveni kufikia Jumatatu saa tatu asubuhi kutokana na tabia yake inayokiuka misingi ya udiplomasia basi atatakiwa kuondoka Uganda mara moja.

Muhoozi ambaye ni mwanae Rais Museveni, amesema kuna ushahidi kuwa balozi wa Marekani amekuwa akitekeleza njama dhidi ya serikali ya chama tawala NRM. Amesema watu wa Uganda hawatakubali kudhalilishwa na kwamba ni bora kujitolea muhanga kuliko kuwa mtumwa.

Katika miezi ya hivi karibuni Marekani imewawekea vikwazo maafisa kadhaa wa Uganda baada ya nchi hiyo kupitisha sheria kali za kuwaadhibu watu wenye uhusiano wa jinsia moja.